
Dar es Salaam. Taasisi ya Utamaduni na Maendeleo Afrika Mashariki (CDEA) imeendelea kuhamasisha matumizi ya urithi wa Afrika katika usanifu wa majengo na ubunifu wa ndani (interior design), kwa lengo la kuhakikisha utambulisho wa Mwafrika unazingatiwa katika ujenzi wa Afrika ya sasa na kizazi kijacho.
Akizungumza katika Jukwaa la Mashariki Creative Economy Expo 2026 linalofanyika Mlimani City na kutarajiwa kuhitimishwa Agosti 21, Meneja Mradi wa CDEA, Angela Kilusungu, amesema mjadala huo umewakutanisha wabunifu na wataalamu wa usanifu kutoka Tanzania na Kenya ili kujadili namna urithi wa Afrika unavyoweza kuwa sehemu ya usanifu wa majengo na mapambo ya ndani.
Kilusungu amesema sekta ya ujenzi imekuwa ikielekea zaidi kwenye usanifu wa kisasa unaosisitiza muonekano wa clean architecture, huku wakati mwingine ukisahaulika matumizi ya nyenzo na alama zinazobeba utamaduni wa Afrika, ikiwemo udongo, vinyago, mbao, michoro na kazi mbalimbali za mikono.

Amesema lengo si kurudi nyuma, bali kujifunza namna jamii za Kiafrika zilivyotumia rasilimali na ubunifu wao katika kujenga mazingira yenye utambulisho, kisha kuendeleza maarifa hayo kwa kutumia teknolojia na ubunifu wa kisasa.
«“Tunaangalia jinsi gani African heritage inaweza kuwa sehemu ya dhima nzima ya majengo yetu tunayojenga. Tunajua sekta ya majengo imegubikwa na watu wanaosema clean architecture, wakisahau kutumia udongo, urembo kama vinyago na vitu vingine vya utamaduni wetu,” amesema Kilusungu.»
Amesema katika jukwaa hilo pia wameshirikisha wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi ambao wamepata fursa ya kubadilishana uzoefu na wataalamu, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya vijana katika kujenga Afrika ya kesho.

Aidha, amesema mjadala mwingine katika jukwaa hilo unahusu namna wasanii na wabunifu wanavyoweza kunufaika na kazi zao hata baada ya kazi hizo kuuzwa kwa mara ya kwanza.
Ameeleza kuwa iwapo kazi ya sanaa inanunuliwa na baadaye kuuzwa tena kwa thamani kubwa, kuna umuhimu wa kuhakikisha msanii aliyeiunda anapata manufaa yanayostahili kwa mujibu wa sheria ya hakimiliki.
Kwa upande huo, wataalamu kutoka COSOTA pamoja na wabunifu ambao kazi zao zimewahi kuuzwa zaidi ya mara moja wamealikwa kujadili utekelezaji wa haki hizo, huku mgeni kutoka Kenya akishirikisha uzoefu wa namna kazi za wabunifu zilivyoweza kuingia katika masoko ya mitaji, ikiwemo kupitia Nairobi Securities Exchange.

Kilusungu amesema mjadala huo unalenga kuwafanya wabunifu waone fursa zilizopo katika masoko mbalimbali na namna wanavyoweza kuongeza thamani ya kazi zao badala ya kutegemea mauzo ya awali pekee.
Katika hatua nyingine, amesema jukwaa hilo limeandaa banda maalumu la vijana litakalotumia teknolojia ya Augmented Reality (AR) kuwawezesha washiriki kutazama namna teknolojia inavyoweza kutumika katika kufikiria mustakabali wa Afrika.
Amesema pia kuna eneo lililoandaliwa kwa kutumia kazi za wabunifu wanaofanya kazi za mikono, likilenga kuonyesha kwa vitendo namna Mwafrika anavyoweza kutumia mbao, michoro na kazi za wasanii wa ndani katika kuboresha na kuongeza thamani ya mazingira ya kuishi.
Kilusungu amesema Tanzania pia inapaswa kuangalia uwezekano wa kuimarisha mfumo wa kitaaluma na kitaasisi kwa wabunifu wa interior design, ikiwemo suala la usajili, ili kuziba pengo lililopo katika sekta hiyo na kuweka mazingira bora kwa wataalamu kufanya kazi kwa viwango vinavyotambulika.
Kwa upande wake Kwa Upande wake Prof,Saudini Mwakaje Mwenyekiti wa Bodi Baraza la Sanaaa Tanzania ( BASATA) amesema Jukwaa hilo litachangia muktadha wa Sheria wa kulinda kazi za ubunifu kufikia malengo ya kiuchumi kutokana na ubunifu mbalimbali.
Naye Scolastika Mandwa Mjumbe wa Chama Cha wabunifu majengo Tanzania Amesema Jukwaa hilo litasaidia kutumia sanaa za ubunifu majengo watarudhisha kwa kizazi kimoja hadi kingine
Mashariki Creative Economy Expo 2026 inaendelea Mlimani City, Dar es Salaam, ikiwa na washiriki kutoka sekta mbalimbali za ubunifu, sanaa, usanifu na uchumi wa ubunifu, huku ikilenga kuibua fursa za kiuchumi kupitia ubunifu na urithi wa Afrika.