×

Ally Kamwe Atoa Onyo kwa Mashabiki “Tusipoe, Hakuna Kuridhika”

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kutoridhika na matokeo mazuri ya mwanzo wa msimu, akisema timu bado haijafikia kiwango kinachohitajika na benchi la ufundi.

Kamwe amesema Yanga bado ipo katika hatua za kujenga mfumo wa uchezaji unaotakiwa na kocha, huku akiwataka mashabiki kutoweka presha kutokana na kauli za wachambuzi wala kulewa sifa.

Amesema kwa makadirio, Yanga bado ipo katika takribani asilimia 25 ya kiwango ambacho benchi la ufundi linataka kukifikia, hivyo kocha anatakiwa kupewa muda wa kuendelea kuboresha timu.
“Timu yetu bado. Tusiingie presha ya wachambuzi na wala tusilewe sifa. Yanga bado kufika kwenye ubora unaosemwa au kuandikwa hivi sasa.”

Ameongeza:
“Kama ni asilimia ndio kwanza tuko asilimia 25 ya kile benchi la ufundi inachokitaka kitokee uwanjani. Tumpe muda kocha wetu Mangoba Mpiga Miti aendelee kuweka mambo sawa katika uwanja wa mazoezi.”

Kamwe pia amewataka mashabiki kuendelea kuwapa nguvu wachezaji ili waweze kuelewa na kutekeleza mipango ya benchi la ufundi, akiamini hilo litasaidia kujenga muunganiko mzuri wa timu.

Akizungumzia mfumo wa uchezaji wa Yanga, amesema mashabiki tayari wameanza kuuona, lakini unahitaji wachezaji kufanya kazi kwa bidii na kukimbia zaidi uwanjani.

Pia amesisitiza umuhimu wa mashabiki kujaza viwanja na kushangilia timu mwanzo hadi mwisho, akisema hamasa yao inaweza kuwa sehemu muhimu ya kuifanya timu iendelee kucheza kwa kasi.

Kamwe ametoa mfano wa mchezo uliopita, akisema baada ya Yanga kupata mabao matatu, baadhi ya mashabiki walipunguza hamasa na kuanza kutumia simu badala ya kuendelea kushangilia.
“Jana, baada ya chuma 3 ni kama tuliridhika majukwaani na tukaanza kuangalia mpira kwa kuchezea simu. Hii ni SUMU KUBWA. Tukipoa sisi, kila kitu kinapoa.”

Ameongeza kuwa wachezaji wanahitaji kusikia sauti za mashabiki ili waendelee kuwa katika kasi kubwa kwa muda wote wa mchezo.
“Kama Kocha anataka timu isipoe, kwanini sisi tunapoa? Tusipoe. Hakuna kuridhika. Tutashika simu zetu mechi ikiisha.”

Kamwe amesema anaamini mashabiki na wanachama wa Yanga wataongeza hamasa katika mchezo unaofuata Jumatatu, huku akihitimisha ujumbe wake kwa kauli ya “Daima Mbele Nyuma Mwiko.”

Leave a Comment