DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imefanya hafla ya kumuaga Balozi Mhandisi Zena A. Said, kufuatia uteuzi wake kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Saudi Arabia.
Hafla hiyo ilifanyika Agosti 21, 2026, huku TIRA ikimpongeza Balozi Zena kwa mchango wake katika kuhamasisha matumizi ya bima na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa sekta hiyo.
Balozi Zena amekuwa Mwenyekiti wa Mabalozi wa Bima tangu mwaka 2023, nafasi ambayo aliitumia kuhamasisha wananchi kuelewa na kutumia huduma za bima.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Zena alisema kupitia nafasi yake kama Balozi wa Bima amepata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali kuhusu sekta hiyo, ikiwemo masuala ya bima na utatuzi wa migogoro.

Aliipongeza TIRA kwa kazi inayofanya kwa kushirikiana na kampuni za bima na kuhimiza sekta hiyo kuendelea kubuni bidhaa na vifurushi vinavyokidhi mahitaji mbalimbali ya Watanzania.
Ametolea mfano bidhaa za Takaful, zinazozingatia misingi ya Sharia, akisisitiza umuhimu wa kuwa na huduma za bima zinazowafikia watu wenye mahitaji na mitazamo tofauti.
Kwa upande wake, Kamishna wa Bima, Dkt. Saqware, ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Balozi Zena, ikiwemo kusukuma ajenda ya bima ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi.
Dkt. Saqware amewataka Mabalozi wa Bima kuendelea kuwa chachu ya maendeleo ya sekta hiyo nchini na kuendeleza juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima.

Naye Msuluhishi wa Migogoro ya Bima, Bi. Margaret Mngumi, amemshukuru Balozi Zena kwa hekima, uvumilivu na mchango wake katika kuimarisha ushirikiano na maridhiano ndani ya sekta ya bima.
Kwa niaba ya ATI, Bi. Flora Minja amemshukuru Balozi Zena kwa uongozi wake na kuahidi kuendelea kushirikiana na Mwenyekiti mpya wa Mabalozi wa Bima katika kuendeleza sekta hiyo.
Naye Naibu Kamishna wa Bima, Bi. Khadija Said, amemshukuru Balozi Zena kwa kujitoa kwake katika shughuli mbalimbali za TIRA, akiahidi kuwa mamlaka hiyo itaendeleza kazi njema iliyoanzishwa chini ya uongozi wake.
Kwa sasa, nafasi ya Mwenyekiti wa Mabalozi wa Bima inatarajiwa kuendelezwa na Mansura Mossi Kassim, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
