×

Msiba Kibaha: Polisi Wawili Wapoteza Maisha Kwa Kugongwa na Gari, Waagwa Tumbi

Pwani. Jeshi la Polisi limewapoteza askari wake wawili katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Maili Moja, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, baada ya kugongwa na gari wakati wakiwa katika eneo la kivuko cha watembea kwa miguu.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa Agosti 25, 2026, majira ya saa 1:40 katika barabara kuu ya Dar es Salaam–Morogoro.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T.804 ERM, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Mlandizi, liliwagonga watembea kwa miguu katika eneo la zebra.

Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Josia Isaya Arute, mwenye umri wa miaka 34, mkazi wa Mlandizi.

Inadaiwa kuwa wakati dereva huyo akifika katika eneo hilo, magari kadhaa yalikuwa yamesimama ili kuwawezesha watembea kwa miguu kuvuka. Hata hivyo, gari hilo lilipita upande wa magari hayo na kuwagonga waliokuwa wakivuka.

Miongoni mwa waliogongwa walikuwa askari wawili wa Polisi, Izdory George Michael na Rehema Juma Magawa.

Izdory alifariki dunia kutokana na ajali hiyo, wakati Rehema alipata majeraha kichwani na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi kwa ajili ya matibabu.

Kwa bahati mbaya, Rehema alifariki dunia asubuhi ya Agosti 26, 2026, wakati akiendelea kupata matibabu.

Baada ya ajali, dereva wa gari hilo aliondoka katika eneo la tukio. Polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanya msako na kulifanikiwa kulikamata gari hilo katika eneo la Kwa Mfipa, Kibaha, likiwa limefichwa.

Gari hilo limepelekwa Kituo cha Polisi Kibaha kwa ajili ya uchunguzi na hatua zaidi za kisheria.

Askari hao wameagwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi kabla ya kusafirishwa kwenda mikoani kwa ajili ya mazishi.

Ibada hiyo ya kuaga imeongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase, na kuhudhuriwa na askari wa vyeo mbalimbali pamoja na ndugu na waombolezaji.

Mwili wa Rehema Juma Magawa umepelekwa Korogwe, Tanga, huku mwili wa Izdory George Michael ukisafirishwa kwenda Sumbawanga Vijijini, Rukwa, ambako mazishi yao yatafanyika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limeendelea kutoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuheshimu alama za barabarani, hususan maeneo ya vivuko vya watembea kwa miguu, ili kuepusha vifo na majeraha yanayotokana na ajali.

Leave a Comment