×

Kampeni Ya Tumaini Ya Yas Yaanza Ubungo, Wajawazito Wanufaika

Dar es Salaam, 28 Agosti 2026 – Wajawazito wanaopata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, watanufaika na vifaa vya kujifungulia pamoja na vifaa tiba vilivyotolewa na wafanyakazi wa Yas Tanzania kupitia Kampeni ya Tumaini, katika jitihada za kuwashika mkono akina mama wajawazito.

Msaada huo umetolewa kupitia Kampeni ya Tumaini, mpango ulioanzishwa na wafanyakazi wa Yas Tanzania, ambao umeanza katika Hospitali ya Wilaya ya Ubungo na unatarajiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Kupitia kampeni hiyo, Yas Tanzania imekabidhi vifaa vya kujifungulia, khanga, vitanda vya uchunguzi kwa wajawazito, mashuka, aproni pamoja na viti mwendo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Yas Tanzania, Caroline Kavishe, alisema kampeni hiyo ni wazo la wafanyakazi wa Yas ambao wameamua kutumia nguvu zao za pamoja kufanya jambo lenye manufaa kwa jamii.
“Tumaini ni kampeni inayoendeshwa na wafanyakazi wetu. Wamechagua kusimama pamoja na akina mama wajawazito kwa kutambua ugumu wa nyakati ambazo wanapitia katika kumleta mtoto duniani. Tunataka wafanyakazi wetu wajivunie si tu kwa kazi wanayofanya, bali pia mchango chanya wanaoweza kuuleta katika jamii,” alisema Kavishe.

Kavishe alisema kampeni hiyo pia inalenga kutambua mchango mkubwa wa madaktari, wauguzi na watoa huduma wengine wa afya ambao kila siku wanawahudumia wajawazito, akina mama na watoto wachanga.

Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano ya Nje wa Yas Tanzania, Rukia Mtingwa, alisema wazo la kampeni hiyo limetokana na kutambua umuhimu wa kusimama pamoja na akina mama katika kipindi muhimu cha ujauzito na kujifungua.
“Kila mama anayekwenda hospitali kujifungua anakwenda na tumaini la kujifungua salama, kumbeba mtoto wake mikononi na kurudi naye nyumbani. Tukajiuliza, katika safari hii muhimu ya mama na mtoto, sisi tunaweza kufanya nini? Ndiyo maana tumeunganisha nguvu zetu na kuanza hapa Ubungo,” alisema Mtingwa.

Akizungumzia dhamira ya Yas kwa jamii, Mtingwa alisema kampuni hiyo inaangalia wajibu wake kwa upana zaidi ya kutoa huduma za mawasiliano na teknolojia.
“Tunaposema Mtandao wa Viwango, kwetu si suala la simu, intaneti na teknolojia pekee. Vilevile, ni suala la viwango vya namna tunavyowajibika kwa jamii. Tunataka popote Yas ilipo, jamii ihisi uwepo wetu kupitia mambo yanayogusa maisha yao,” alisema.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Dkt. Chrispin Kayola, alisema vifaa hivyo vitaongeza uwezo wa hospitali katika kuwahudumia wajawazito na akina mama wanaofika kujifungua.
“Tunapokea wajawazito karibu 150 kwa mwezi katika kipindi kama hiki cha low season, na nusu kati yao huhitaji huduma za upasuaji. Hivyo, vifaa hivi vina umuhimu mkubwa sana kwa hospitali yetu. Vitasaidia kuwaongezea watoa huduma wetu nyenzo wanazohitaji kuwahudumia akina mama,” alisema Dkt. Kayola.

Kampeni ya Tumaini inatarajiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwapa wafanyakazi wa Yas Tanzania nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika kusaidia jamii, huku wajawazito na akina mama wakiwa miongoni mwa walengwa wa kampeni hiyo.

Leave a Comment