Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, amezitaka nchi za Kiislamu kuungana dhidi ya Marekani na Israel, akizitaja nchi hizo mbili kuwa ni maadui wa ulimwengu mzima wa Kiislamu.
Katika ujumbe uliochapishwa na Shirika la Habari la Iran (IRNA), Khamenei ametoa wito kwa mataifa ya Kiislamu kutambua kile alichokiita kuwa ni “adui wao wa kweli” na kuchukua hatua za kuzuia mipango yake.
Kauli hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Iran, Marekani na Israel ukiendelea kuwa mkubwa, huku Tehran ikisisitiza umuhimu wa mshikamano miongoni mwa nchi za Kiislamu.
Khamenei hajawa akionekana hadharani tangu alipoteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa Iran mwezi Machi, na hivyo ujumbe huo kuwa miongoni mwa taarifa zake chache zilizotolewa hadharani tangu achukue nafasi hiyo.
Wakati huo huo, meli ya kivita ya Marekani, USS Abraham Lincoln, imepita nchini Singapore ikiwa njiani kurejea Marekani baada ya kukamilisha operesheni ya muda mrefu katika Mashariki ya Kati.
Meli hiyo inatarajiwa kusimama nchini Thailand kwa mapumziko kabla ya kuendelea na safari yake kuelekea kituo chake cha kijeshi nchini Marekani.
