
Dar es Salaam, Septemba 4, 2026 — Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc imeingia ubia wa miaka mitatu na Bridge for Billions, mtandao wa kimataifa wa ujasiriamali, kwa lengo la kuimarisha mfumo wa ujasiriamali na kuongeza fursa za ukuaji kwa biashara changa nchini Tanzania.
Kupitia mpango huo unaotekelezwa chini ya Vodacom Digital Accelerator (VDA), taasisi zinazosaidia wajasiriamali nchini zitawezeshwa ili kuongeza uwezo wa kuwasaidia waanzilishi wa biashara kukuza na kupanua shughuli zao.

Ushirikiano huo unalenga kuwafikia zaidi ya wajasiriamali 1,000 na kusaidia zaidi ya biashara 40 kukua na kupanuka katika kipindi cha miaka mitatu.
Tofauti na awamu zilizopita ambazo VDA ilijikita zaidi katika kusaidia biashara changa moja kwa moja, mpango huo sasa utawekeza pia katika taasisi zinazowasaidia wajasiriamali, ikiwemo vituo vya kulea na kukuza biashara, vyuo vikuu, vituo vya ujasiriamali na mashirika ya maendeleo ya biashara.
Kupitia ushirikiano huo, Bridge for Billions italeta utaalamu katika programu za kulea na kukuza biashara changa, teknolojia za kidijitali pamoja na ujenzi wa uwezo wa taasisi zinazohudumia wajasiriamali.
Taasisi zitakazochaguliwa zitapatiwa mafunzo maalumu na zitawezeshwa kutumia zana na mifumo mbalimbali ya Bridge for Billions, sambamba na kupata msaada katika kubuni na kuendesha programu za ujasiriamali.

Aidha, taasisi hizo zitaunganishwa na mtandao wa kimataifa wa washauri na taasisi zinazosaidia wajasiriamali, hatua inayolenga kuwezesha kubadilishana uzoefu, maarifa na fursa za ushirikiano.
Wajasiriamali watakaopatikana kupitia taasisi hizo watapitia mchakato maalumu wa kulea na kukuza biashara zao. Biashara zitakazoonyesha uwezo mkubwa wa kukua zitaendelea kwenye hatua ya acceleration, ambapo zitapatiwa msaada wa kina zaidi katika upanuzi wa biashara na maandalizi ya fursa za uwekezaji.
Vodacom Digital Accelerator ilianzishwa mwaka 2019 na imekuwa ikisaidia biashara changa na zinazokua zinazotumia teknolojia kutengeneza bidhaa na huduma zenye uwezo wa kufikia masoko mapana.
Kupitia programu hiyo, wajasiriamali wamekuwa wakipata mafunzo, ushauri wa kitaalamu, teknolojia, fursa za kuunganishwa na wawekezaji pamoja na kufikia mitandao na washirika wa Vodacom.
Programu hiyo imewahi kusaidia wajasiriamali wanaofanya shughuli katika sekta mbalimbali, zikiwemo afya, kilimo, elimu na huduma za kifedha.
Kwa ubia huu mpya, Vodacom na Bridge for Billions wanalenga kuifanya Tanzania kuwa na mfumo imara zaidi wa kuwalea na kuwawezesha wajasiriamali, huku wakiongeza uwezo wa biashara changa kukua na kuchangia katika uchumi.
Kundi la kwanza la taasisi zitakazoshiriki katika mpango huo linatarajiwa kutangazwa Oktoba 2026, huku maombi kwa wajasiriamali yakitarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa Septemba 2026.