
Dar es Salaam. Watu wanne wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Abood kugongana na gari dogo aina ya Toyota IST katika eneo la Bunju Sokoni, Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania leo, Septemba 8, 2026, ajali hiyo ilitokea Septemba 7, 2026 saa 7:40 usiku katika Barabara ya Bagamoyo, eneo la Bunju Sokoni.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa basi lenye namba za usajili T 235 EMJ, aina ya Yutong mali ya kampuni ya Abood, lilikuwa likiendeshwa na Christivian Steven Shemuhilu, mwenye umri wa miaka 38, mkazi wa Kange, Tanga.
Basi hilo lilikuwa likitokea Tegeta kuelekea Bunju likiwa safarini kwenda Mkoani Tanga, ndipo lilipogongana na gari lenye namba T 274 ERU, aina ya Toyota IST, lililokuwa likiendeshwa na Hamad Mohamed Juma, mwenye umri wa miaka 37, mkazi wa Mtoni Mtongani, Dar es Salaam.
WATU WANE WAFARIKI
Jeshi la Polisi limesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi, ambaye alifanya kitendo cha “overtake” bila kuchukua tahadhari dhidi ya watumiaji wengine wa barabara.
Watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni:
- Hamad Mohamed Juma, miaka 37, mkazi wa Mtoni Mtongani, Dar es Salaam.
- Edward Kimanyara, mstaafu, mkazi wa Yombo Dovya, Temeke.
- Magdalena Manyenga, miaka 45, mkazi wa Temeke.
- Melina Emmanuel Kayoka, miaka 42, mkazi wa Yombo Kisiwani, Temeke.
Jeshi la Polisi limesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Kinondoni, Dar es Salaam.
DEREVA AKAMATWA
Dereva wa basi hilo, Christivian Steven Shemuhilu, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa watumiaji wote wa barabara, hususan madereva, kuhakikisha wanaendesha kwa umakini, kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali na madhara kwa watumiaji wengine.