×

Mahakama Yaagiza IGP, CDF NA DCI Kutoa Ushahidi Kesi Ya Uhaini Ya Tundu Lissu

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imeagiza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) pamoja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuitwa kutoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Uamuzi huo umetolewa leo, Septemba 10, 2026, na Jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, baada ya Lissu kuwasilisha orodha ya mashahidi anaotaka watoe ushahidi katika kesi hiyo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura.

Miongoni mwa mashahidi waliotajwa na upande wa utetezi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan; aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango; aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Mkuu wa Majeshi, Jenerali John Jacob Mkunda; IGP; Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa; DCI Ramadhani Kingai; pamoja na John Mnyika, Amani Golugwa, John Heche na Brenda.

Hata hivyo, Mahakama imekataa ombi la kuwaita Rais Samia Suluhu Hassan, Dkt. Philip Mpango, Kassim Majaliwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa kutoa ushahidi.

Mahakama imeeleza kuwa si sahihi kuwaita mashahidi hao kwa madhumuni ya kuthibitisha iwapo walitishika au hawakutishika kutokana na kauli zinazolalamikiwa katika shauri hilo.

Mkuu wa Majeshi, Jenerali John Jacob Mkunda.

Katika uamuzi huo, Mahakama imekumbusha kuwa Agosti 21, 2026, ilitoa uamuzi mdogo kwamba mshtakiwa ana kesi ya kujibu na kumweleza kuwa ana haki ya kuleta mashahidi wake.

Baada ya kuwasilisha orodha hiyo, upande wa utetezi uliiomba Mahakama kutoa wito kwa mashahidi hao ili wafike mahakamani na kutoa ushahidi.

Kwa upande mwingine, Mahakama imekubali kuitwa kwa Mkuu wa Majeshi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, hatua inayowaruhusu kufika mahakamani kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Kesi hiyo inaendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Leave a Comment