DUBAI: Kampuni ya Mkuyu Africa imewakutanisha Watanzania wanaoishi na kufanya shughuli mbalimbali nchini Dubai, ikiwa na lengo la kuwajengea uelewa kuhusu fursa za uwekezaji nchini Tanzania, hususan katika sekta ya ardhi, majengo na mali isiyohamishika.
Hatua hiyo imekuja wakati biashara na mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na Dubai yakiendelea kukua, huku Watanzania wengi wakifika katika Falme za Kiarabu kutafuta fursa za biashara na kujenga mitaji.
Katika kuunga mkono jitihada hizo, Mkuyu Africa iliandaa kongamano lililowakutanisha wafanyabiashara wadogo wenye asili ya Tanzania wanaoishi Dubai, ambapo walijadili namna wanavyoweza kutumia fursa wanazozipata ughaibuni kuwekeza nchini.
Kongamano hilo pia lililenga kuwapa washiriki uelewa kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya ujenzi na mali isiyohamishika, pamoja na namna Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanavyoweza kumiliki mali nchini kupitia mifumo rasmi ya kifedha.

Mkuyu Africa: Tanzania imebadilika kwa kasi
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa Mkuyu Africa, Juneid Othman, alisema Watanzania waliotoka nchini miaka 10 iliyopita wanaweza kushangazwa na kasi ya maendeleo iliyopatikana katika sekta ya ujenzi.
Alisema sekta hiyo imekua kwa kiasi kikubwa, ikiwemo ujenzi wa majengo ya biashara, nyumba za makazi na miradi ya nyumba za kupangisha, hususan katika maeneo ya kibiashara kama Kariakoo na maeneo ya makazi ya hadhi ya juu kama Masaki.
“Ukitoka Tanzania miaka 10 iliyopita na ukarudi leo, unaweza kushangazwa na mabadiliko makubwa yaliyotokea katika sekta ya ujenzi. Kuna maendeleo makubwa katika ujenzi wa majengo ya biashara, makazi na nyumba za kupangisha,” alisema.
Juneid alisema mazingira ya uwekezaji yanaendelea kutoa fursa kwa Watanzania kumiliki mali kupitia benki na taasisi mbalimbali za kifedha.
Alitaja miradi ya Mkuyu Africa katika maeneo ya Kariakoo na Masaki, akisema kampuni hiyo inaendelea kushiriki katika ujenzi na uendelezaji wa majengo ya mali nchini kama sehemu ya maandalizi ya maisha yao ya baadaye na kuweka urithi kwa viz makazi na biashara.
Kwa mujibu wa Juneid, Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanaweza kutumia fursa hizo kujenga mali nchini kama sehemu ya maandalizi ya maisha yao ya baadaye na kuweka urithi kwa vizazi vijavyo.
Wafanyabiashara Dubai wataka kuwekeza Tanzania
Mfanyabiashara wa bidhaa za thamani na mapambo ya ndani nchini Dubai, Ashraf Mohamud, alisema Watanzania wengi wanaoishi Dubai wanaendelea kufanya biashara huku wakitafuta mitaji kwa lengo la kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Alisema ujio wa Mkuyu Africa nchini Dubai umewapa motisha na taarifa zaidi kuhusu fursa zilizopo Tanzania, jambo ambalo linawasaidia kupanga kwa umakini namna ya kuanza kuwekeza nyumbani.
“Tumekuja Dubai kutafuta maisha na kufanya biashara, lakini moja ya malengo yetu ni kupata mtaji na kuja kuwekeza nyumbani. Ujio wa Mkuyu Africa umetupa hamasa na kutufanya tuanze kufikiria kwa umakini zaidi kuhusu uwekezaji nchini,” alisema.
Watanzania Dubai wataja changamoto ya kuwekeza nyumbani
Ashraf alisema baadhi ya Watanzania wanaoishi Dubai wamekuwa wakikumbana na changamoto katika uwekezaji, hasa pale wanapowatuma ndugu zao fedha kwa ajili ya kununua ardhi au kujenga nyumba nchini.
Alisema hali hiyo imewafanya baadhi yao kutafuta njia mbadala zitakazowawezesha kufanya uwekezaji moja kwa moja na kwa utaratibu unaoeleweka.
“Watanzania wengi wanaoishi huku wanatamani kuja kuwekeza nchini, lakini hapo awali kumekuwa na changamoto na wakati mwingine urasimu, hasa pale tunapowatuma ndugu zetu fedha kwa ajili ya uwekezaji,” alisema.
Aliongeza kuwa fursa zinazotolewa na kampuni kama Mkuyu Africa, ikiwemo uwezekano wa kumiliki mali kupitia taasisi za kifedha na kufanya malipo kwa awamu kulingana na masharti yaliyowekwa, zinaweza kuwasaidia Watanzania waishio nje ya nchi kuwekeza kwa utaratibu rasmi.
Kwa mujibu wa washiriki wa kongamano hilo, uwekezaji nchini Tanzania unaweza kuwa sehemu ya kujenga maisha ya baadaye, kuongeza thamani ya mitaji na kuweka msingi wa mali kwa ajili ya familia na vizazi vijavyo.
