
Familia, marafiki, waumini wa dini, viongozi wa serikali na maelfu ya waombolezaji leo, Alhamisi Oktoba 8, 2026, wamekusanyika katika nyumba ya familia ya Chivayo iliyopo Gletwyn, Harare, Zimbabwe, kutoa heshima za mwisho kwa mfanyabiashara Wicknell Chivayo na mkewe, Lucy “Lulu” Muteke.

Ibada na shughuli za kuaga zimeendelea huku waombolezaji wakifika kwa wingi kuungana na familia katika kipindi hiki cha majonzi, kabla ya miili ya wanandoa hao kusafirishwa kwenda Glen Forest Memorial Park kwa ajili ya mazishi.
Miongoni mwa waliohudhuria ni mwanamuziki Selmor Mtukudzi pamoja na mumewe, Tendai Manatse, ambao wamejiunga na waombolezaji wengine kutoa heshima zao za mwisho kwa Chivayo na Lucy.

Hudhurio la Selmor linakuja baada ya Chivayo hivi karibuni kuweka sharti katika zawadi alizokuwa amemwahidi mwanamuziki huyo, akimtaka kwanza kupatana na mama yake wa kambo, Daisy Mtukudzi. Hatua hiyo ilichangia Selmor na Daisy kukutana na kuanza mchakato wa kusuluhisha tofauti zao.

Chivayo na Lucy wanatarajiwa kuzikwa leo katika Makaburi ya Glen Forest Memorial Park jijini Harare, baada ya familia na waombolezaji kukamilisha maandalizi ya mwisho ya mazishi.
Wanandoa hao walifariki pamoja na watu wengine watatu katika ajali ya helikopta iliyotokea Septemba 30, 2026, katika eneo la Kudenga Farm, Marondera, takribani kilomita 70 mashariki mwa Harare.
Jana, Jumatano Oktoba 7, miili ya Chivayo na Lucy ilichukuliwa katika kituo cha kuhifadhi miili cha Doves Funeral Services katikati ya Harare na kupelekwa katika nyumba ya familia yao iliyopo Gletwyn, ambako iliwekwa kwa ajili ya waombolezaji kutoa heshima zao za mwisho.

Msafara wa kupeleka miili hiyo ulivuta umati mkubwa wa watu katika mitaa ya Harare. Polisi walifunga baadhi ya barabara kuu ili kuruhusu msafara huo kupita.
Maelfu ya watu walijipanga kandokando ya barabara kushuhudia msafara huo, huku baadhi wakiwa wamevalia mavazi meupe na wengine wakirekodi tukio hilo kwa simu zao.
Kwa sasa, waombolezaji wanaendelea kukusanyika Gletwyn huku familia ikiendelea na taratibu za mwisho kabla ya safari ya mwisho ya Chivayo na Lucy kuelekea Glen Forest Memorial Park.





