
Mwili wa Jane Urassa umefikishwa leo, Oktoba 8, 2026, katika Kanisa la KKKT Mbezi Beach, Dar es Salaam, kwa ajili ya ibada ya kuaga kabla ya kusafirishwa kuelekea Machame, mkoani Kilimanjaro, ambako anatarajiwa kuzikwa kesho, Ijumaa Oktoba 9, 2026.
Wasifu wa marehemu Jane Urassa umesomwa katika ibada hiyo, huku akielezwa na waliomfahamu kama mtu mpole, mnyenyekevu na mpenda amani.
Jane alifariki dunia alfajiri ya Oktoba 1, 2026, katika nyumba yao iliyopo Bunju B, Dar es Salaam, katika tukio linalodaiwa kuhusisha kupigwa risasi. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, tukio hilo linadaiwa kumhusisha mumewe, Laurent Kweka.
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi, baada ya ibada ya kuaga jijini Dar es Salaam, mwili wa Jane utasafirishwa kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.
Mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho katika Kijiji cha Nkuu Sinde, Kata ya Machame Mashariki, Wilaya ya Hai, eneo ambalo ni upande wa familia ya marehemu.
Familia, ndugu, marafiki na waombolezaji wamekusanyika katika Kanisa la KKKT Mbezi Beach kumuaga Jane kabla ya mwili wake kusafirishwa kuelekea Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.