×

Stanbic Yatoa Vifaatiba vya Milioni 40 Kuboresha Huduma za Afya Kigamboni

Benki ya Stanbic Tanzania imekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 40 kwa Hospitali ya Vijibweni, Kigamboni, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuchangia uboreshaji wa huduma za afya, hususan huduma za uzazi, uangalizi wa wagonjwa na upimaji wa afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Msaada huo ni mwendelezo wa juhudi za Stanbic katika kusaidia maendeleo ya jamii wilayani Kigamboni. Awali, kupitia mpango wa Stanbic Madawati, benki hiyo ilitoa madawati 150 yenye thamani ya shilingi milioni 20 kwa Shule ya Msingi Ufukoni, sambamba na kupanda miti 150 wilayani humo.

Vifaa hivyo vinatarajiwa kusaidia kuboresha huduma mbalimbali zinazotolewa hospitalini hapo. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vitanda vitano vya wagonjwa, kitanda kimoja cha kujifungua, mashine ya kufuatilia hali ya mgonjwa, mashine 30 za kupima shinikizo la damu na vifaa vingine vya matibabu. Benki pia imetoa vifaa vya usafi na kompyuta zitakazosaidia katika utunzaji wa kumbukumbu na uendeshaji wa shughuli za hospitali.

Vifaa hivyo vinatarajiwa kuongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma kwa wakati na kwa ufanisi zaidi. Vitanda vipya vitasaidia kuboresha huduma kwa wajawazito na wagonjwa wanaohitaji kulazwa, huku mashine za kufuatilia hali ya wagonjwa na kupima shinikizo la damu zikitarajiwa kurahisisha upimaji na uangalizi wa wagonjwa katika hospitali hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Maalum wa Stanbic Bank Tanzania, Bw. Omari Mtiga, alisisitiza dhamira ya benki hiyo ya kuchangia ustawi wa jamii kupitia uwekezaji katika huduma muhimu.

“Upatikanaji wa huduma bora za afya ni msingi muhimu wa kujenga jamii yenye afya, nguvu kazi imara na maendeleo endelevu. Kwa Stanbic, tunaamini wajibu wetu hauishii katika kutoa huduma za kifedha, bali pia kuchangia maendeleo na ustawi wa jamii tunazozihudumia.

“Kupitia msaada huu, tunalenga kuwawezesha wataalamu wa afya kupata vifaa muhimu vitakavyowasaidia kutoa huduma bora na kwa wakati, hususan kwa akina mama na familia zinazotegemea huduma hizi kila siku. Hii ni sehemu ya dhamira yetu ya kwenda hatua ya ziada, Going the Extra Mile, katika kuleta mabadiliko yenye manufaa ya kudumu kwa jamii,” alisema Bw. Mtiga.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Dalmia Mikaya, aliishukuru Benki kwa msaada wake. “Kigamboni inakua kwa kasi, na vituo vyetu vya afya vinahudumia watu wengi kuliko vilivyojengwa kuhudumia. Vifaa hivi vitasaidia kuboresha huduma zinazotolewa kwa wagonjwa na kupunguza changamoto zinazowakabili watumishi wa afya katika kutekeleza majukumu yao.”

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Dkt. Lucas Ngamtwa, alisema vifaa hivyo vitaonekana mara moja katika utendaji wa kila siku wa hospitali. “Kila kifaa kilichotolewa kina umuhimu wa moja kwa moja katika utoaji wa huduma. Vifaa hivi vitatusaidia kufanya vipimo kwa wakati, kuboresha huduma kwa akina mama na kuimarisha uangalizi wa wagonjwa wanaohitaji huduma maalum,” alisema.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Diwani wa kata ya Vijibweni, Bw. Nicholas Mranda, na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya, Bi. Agusta Safari, Pamoja na uongozi wa Hospitali ya Vijibweni na timu ya Stanbic Bank Tanzania.

 

 

Leave a Comment