Mfuko wa uwekezaji wa Zan Timiza Exchange Traded Fund (ETF), unaosimamiwa na Zan Securities Limited, umekusanya shilingi bilioni 9.46 katika mauzo ya awali ya vipande vyake, kiasi kilichozidi lengo la kukusanya shilingi bilioni tano.
Mafanikio hayo yanaonesha fursa zilizopo katika soko la mitaji nchini katika kukusanya fedha za ndani kwa ajili ya uwekezaji na kuchochea maendeleo ya uchumi, huku wananchi wakipata nafasi ya kushiriki katika uwekezaji rasmi kulingana na uwezo wao wa kifedha.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuorodheshwa rasmi kwa mfuko huo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Kamishna wa Fedha za Nje na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Rished Bade, aliyemwakilisha Waziri wa Fedha, amesema mafanikio hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa nchi kukusanya mitaji ya ndani na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya fedha kutoka nje.
Bade amesema Zan Timiza ETF ni mfuko wa uwekezaji wa pamoja unaowekeza katika mifuko mingine ya uwekezaji wa pamoja, huku vipande vyake vikinunuliwa na kuuzwa kupitia soko la hisa, hivyo kupanua fursa kwa wananchi kushiriki katika shughuli za uwekezaji.
Ameitaka Zan Securities Limited, kwa kushirikiana na NMB Bank inayohusika na huduma za utunzaji wa mali za mfuko huo, kuhakikisha fedha za wawekezaji zinasimamiwa kwa uwazi, uadilifu na weledi, kwa kuzingatia sera za uwekezaji, nyaraka za mfuko na miongozo ya mamlaka husika.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Zan Securities Limited, Raphael Masumbuko, amesema kiwango kilichokusanywa kinaonesha mwitikio wa Watanzania katika kutumia fursa za uwekezaji zinazopatikana kupitia soko rasmi la mitaji.
Masumbuko amesema mauzo ya awali ya vipande vya mfuko huo yalianza Agosti 17, 2026 na kufungwa Septemba 17, 2026, huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwa shilingi 20,000 ili kuwawezesha wananchi wa makundi mbalimbali ya kipato kushiriki katika uwekezaji huo.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
