×

Bibi Miaka 78 Afungwa Miaka 30 Jela Kwa Kukutwa Na Bangi Kilo 33.25

MWANZA — Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza imemhukumu Suzana Marwa, maarufu kwa jina la Maswi, mwenye umri wa miaka 78, kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki bangi yenye uzito wa kilogramu 33.25.

Suzana alikamatwa Machi 29, 2026, katika eneo la Bugarika Kaskazini, baada ya maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kufanya upekuzi nyumbani kwake na kukuta bangi hiyo ikiwa imehifadhiwa kwenye mifuko miwili na ndoo ya plastiki.

Hukumu hiyo ilitolewa Septemba 23, 2026, na Hakimu Mkazi Mwandamizi Clement Tuji, ambaye alieleza kuwa umri mkubwa wa mshtakiwa ungeweza kuzingatiwa katika kupunguza adhabu, lakini sheria inayohusika inaweka kifungo cha lazima cha miaka 30 kwa kosa hilo.

Kwa mujibu wa maelezo ya hukumu hiyo, mahakama iliamuru bangi iliyokamatwa iteketezwe, huku fedha taslimu Sh195,000 zilizopatikana wakati wa tukio hilo zikitaifishwa.

Hukumu hiyo inaonesha uzito wa adhabu zinazoweza kutolewa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya nchini Tanzania.

Leave a Comment