
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dodoma, inatarajiwa kutoa hukumu kesho, Ijumaa, Oktoba 16, 2026, katika kesi ya kikatiba Na. 7300 ya mwaka 2026 inayohusu haki ya mawakili kukutana na mteja wao, Tundu Antipas Lissu, gerezani kwa faragha bila kusikilizwa au kuingiliwa na maafisa wa magereza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CHADEMA leo, Oktoba 15, 2026, shauri hilo linahusu masuala muhimu ya kikatiba na kisheria, hususan haki ya mtu kupata ushauri na uwakilishi wa kisheria bila kuingiliwa, pamoja na wajibu wa kulinda usiri wa mawasiliano kati ya wakili na mteja wake.
Hukumu hiyo inatarajiwa kujibu maswali muhimu kuhusu uhalali wa maafisa wa magereza kusikiliza au kuingilia mawasiliano kati ya mawakili na wateja wao wanapokutana kwa madhumuni ya kupata ushauri wa kisheria, pamoja na haki ya mawakili kukutana na wateja wao walioko magerezani bila kuzuiwa kwa namna inayoweza kuathiri haki hiyo.
Shauri hilo linatarajiwa kutolewa hukumu na jopo la majaji watatu, ambao ni Jaji Mruma, Jaji Rumisha na Jaji Longopa.
Katika taarifa hiyo, CHADEMA imewataka wanachama, wafuasi na wananchi wote kufika mahakamani kufuatilia mwenendo wa shauri hilo, ikieleza kuwa uamuzi huo una umuhimu mkubwa katika masuala ya haki za kikatiba na upatikanaji wa haki nchini.
Taarifa hiyo imesainiwa na Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA.
