×

Askari 13 Wakamatwa kwa Tuhuma za Vifo vya Watu Wanne Kagera

BUKOBA: Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limewakamata watuhumiwa 13, wakiwemo askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (TANAPA), askari wa Misitu (TFS) na askari Mgambo, kwa tuhuma za mauaji ya watu wanne yaliyotokea katika Kijiji cha Kanyamika, Kata ya Karambi, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, tukio hilo lilitokea Oktoba 17, 2026, majira ya saa 10:00 asubuhi, katika eneo la Kanyamika, barabara kuu ya Muleba kuelekea Biharamulo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa askari hao walikuwa doria katika pori la hifadhi ya misitu ya Ruiga wakitumia gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili 02 JU 354, mali ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwashambulia watu waliokuwa wamebeba silaha aina ya AK-47 tatu, baada ya kukataa kukamatwa na kujaribu kuwanyang’anya silaha askari hao waliokuwa doria katika eneo hilo.

Kutokana na tukio hilo, watu wanne walifariki dunia. Waliotajwa katika taarifa hiyo ni Osward Yuster (38), mkazi wa Ngote; Pius Charles (40), mkazi wa Magata; Charles Michael (35), mkazi wa Ngote; na Edgar Elias Lukangula (44), mkazi wa Butembo, ambaye alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kagera Oktoba 18, 2026, majira ya alfajiri.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa tukio hilo lilisababisha uharibifu wa gari la Serikali lenye namba za usajili 02 JU 0354, mali ya TFS, ambalo liliharibiwa vioo vya mbele na vya pembeni.

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata pikipiki 10, magari madogo 22, mapanga matano, kofia ngumu mbili, makoti mawili, silaha aina ya AK-47 tatu, maganda ya risasi za AK-47 45 pamoja na gari moja aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili 02 JU 0354, mali ya TFS.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limesema limechukua hatua za kisheria kuhusu tukio hilo na kwamba watuhumiwa wote wamekamatwa kwa ajili ya uchunguzi.

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuzingatia sheria na kuepuka kujichukulia sheria mkononi wanapokutana na askari au mamlaka zilizopewa dhamana ya kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi.

Leave a Comment