
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawasaka wanawake wawili kwa tuhuma za kuhusika katika matukio mawili tofauti ya jinai, likiwemo la kutekwa na kuibiwa kwa mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu katika eneo la Ilemela.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Oktoba 29, 2026, uchunguzi kuhusu matukio hayo unaendelea ili kuwabaini watuhumiwa na kuwachukulia hatua za kisheria.
Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka mwanamke ambaye jina lake na makazi yake bado hayajafahamika, anayetuhumiwa kumuiba mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu.
Tukio hilo limeripotiwa kutokea Oktoba 25, 2026, majira ya saa 7:00 mchana, katika Kanisa la Living Water lililopo Mtaa wa Kiseke A, Kata ya Kiseke, Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mama wa mtoto huyo, Godliver Bahati Zilahenda, mwenye umri wa miaka 23, alikutana na mwanamke huyo kanisani kwa mara ya kwanza Oktoba 18, 2026. Walikutana tena Oktoba 25, 2026 na kukaa pamoja wakati wa ibada.
Ilipofika wakati wa kutoa sadaka, mwanamke huyo alimwomba mama wa mtoto amshikie mtoto wake. Hata hivyo, baada ya mama huyo kurejea kutoka kutoa sadaka, alidaiwa kukuta mwanamke huyo amemchukua mtoto na kuondoka naye kusikojulikana.
Polisi wamesema uchunguzi unaendelea kumsaka mtuhumiwa na kumrejesha mtoto akiwa salama. Jeshi hilo pia limewaomba wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kumpata mwanamke huyo na kuhakikisha usalama wa watoto.
WANAWAKE WAWILI WATUHUMIWA KUTUPA VICHANGA
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linafanya uchunguzi kuhusu kupatikana kwa miili ya vichanga viwili vya jinsia ya kiume vilivyodaiwa kutupwa katika eneo la Nyasaka, Wilaya ya Ilemela.
Tukio hilo limeripotiwa kutokea Oktoba 27, 2026, majira ya saa 12:45 jioni, katika Mtaa wa Chamwenda, Kata ya Nyasaka, ambapo wananchi walitoa taarifa baada ya kuona miili hiyo ikiwa imetelekezwa barabarani.
Baada ya kupokea taarifa hizo, askari Polisi walifika eneo la tukio na kufanya uchunguzi wa awali. Miili hiyo ilichukuliwa na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, vichanga hivyo vinakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miezi mitano hadi sita tangu kutungwa kwa mimba.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini waliohusika na tukio hilo pamoja na chanzo chake, huku likiomba mtu yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi kujitokeza na kutoa ushirikiano.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watakaobainika kuhusika na matukio hayo.

