×

Ajali ya Ndege Yauwa Watu Tisa Baada Kuanguka na Kuteketea Kwa Moto, Gavana wa Florida Afunguka

Watu tisa wamefariki dunia baada ya ndege binafsi waliyokuwa wakisafiria kuanguka katika eneo la Palm Beach, jimbo la Florida nchini Marekani, katika ajali iliyosababisha ndege hiyo kuteketea kwa moto.

Ajali hiyo imetokea Jumapili jioni, Novemba 1, 2026, katika eneo lililopo umbali wa takribani kilomita 12 kutoka makazi ya mapumziko ya Mar-a-Lago yanayomilikiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, ndege hiyo inayodaiwa kuwa aina ya Learjet 60 ilikuwa imebeba watu tisa na ilikuwa ikisafiri kutoka jimbo la Texas kuelekea Bahamas kabla ya kuanguka.

Hadi sasa, utambulisho wa watu waliokuwa ndani ya ndege hiyo haujatangazwa rasmi na mamlaka husika.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA) imesema imetuma timu ya wataalamu katika eneo la tukio kwa ajili ya kufanya uchunguzi utakaobaini chanzo cha ajali hiyo.

Picha zilizopatikana katika eneo la ajali zinaonyesha mabaki ya ndege yaliyoteketea kwa moto pamoja na shimo kubwa lililotokana na nguvu ya ndege kugonga ardhi.

Wakati huohuo, ripoti za vyombo vya habari nchini Marekani pamoja na uchambuzi wa takwimu za safari ya ndege zinaashiria kuwa ndege hiyo ilikuwa ikipoteza mwinuko kwa kasi kubwa, inayokadiriwa kufikia mamia ya futi kwa sekunde, kabla ya kuanguka.

Video ambayo bado haijathibitishwa rasmi na mamlaka, iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kuonekana kurekodiwa kupitia kamera ya gari, inaonyesha ndege hiyo ikianguka kwa ghafla.

Katika video hiyo, magari yanaonekana yakiendelea na safari katika barabara ya makazi kabla ndege hiyo haijaanguka, na muda mfupi baadaye kutokea mlipuko mkubwa ulioambatana na moto na vipande vya mabaki kurushwa hewani.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano ulioitishwa kufuatia ajali hiyo, Gavana wa Florida, Ron DeSantis, amesema video ya tukio hilo inashtua kutokana na namna ndege hiyo ilivyoanguka na kusababisha mlipuko mkubwa.

“Unapoitazama video hii, kwa kweli inashtua sana. Ni kana kwamba kombora linashuka kutoka angani, kisha kunatokea mlipuko mkubwa na vipande vya mabaki kurushwa kila upande,” amesema DeSantis.

Kwa sasa, uchunguzi wa mamlaka za anga unaendelea kubaini mazingira yaliyopelekea ajali hiyo, huku familia za wahanga zikisubiri taarifa rasmi kuhusu utambulisho wa ndugu zao.

Leave a Comment