×

Mbeto: CCM Kitaendelea Kubeba Matumaini ya Watanzania bila Kuyumbishwa

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar,Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis.

Chama Cha Mapinduzi kimewahakikishia Wananchi kuwa kitabaki na umadhubuti wake wa kubeba matumaini ya Wananchi wote bila kujali imani zao za dini,Itikadi za Kisiasa au kabila zao.

Pia chama hicho kimewataka Wananchi kuwa hodari wa kuvipekua Vyama vya Siasa kabla kufikia maamuzi ya kuvifuata , kujiunga navyo na kuviunga mkono .

Maelezo hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar,Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis huku akiwasisitiza Watanzania wote kuendelea kulinda Amani na utulivu wa nchi yao.

Mbeto alisema uzoefu wa CCM katika medani za madaraka, uongozi, kisiasa na kiutawala , ni mkubwa usiolingana na viongozi wa Vyama vingine.

Alisema chama cha Siasa kilichoshika madaraka ya Utawala kwa miaka zaidi ya sitini, bila shaka chama hicho hakifanani kwa lolote na Vyama vichanga vinavyoibuka na kufa kama uyoga nyakati za masika.

“Vyama vingi vitaendelea kuibuka
,kuishi kwa muda ,vitayumba hatimae vitakufa. CCM kwa upeo wa viongozi wake na uzoefu wake kitabaki na uhai wake na kudumu “Alisema Mbeto

Aidha, Katibu huyo Mwenezi,! alieleza ndio maana CCM kinaweza kujadili masuala yake mazito ya kisiasa, kukabiliana na chamgamoto kadhaa za ndani na nje kwa umakini na kufikia kutoa maamuzi magumu.

“Vyama vichanga vyote vya Kisiasa haviwezi kupata ustawi na uwezo wa kuhimili misukosuko . CCM imepitia mengi makubwa lakini hakikutikisika katika kupigania maslahi mapana ya Taifa” Alisema.

Akisisitiza zaidi, Katibu huyo Mwenezi aliendelea kuutaja uzoefu na uwezo mkubwa wa kiutawala na kisiasa, alidai CCM kinapotaka kutoa maamuzi yake ,hutanguliza kwanza utaifa si kitu kingine.

“CCM si chama kinachofuga wanachama mamluki na wasaliti. Ni chama kinachoamini na kufuata Siiasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Hujitegemea kifikra , kimawazo,kiakili na kuamini katika Sera na misimamo yake “Alifafanua Mbeto .

Akizungumza kwa undani, Mbeto alisema CCM hakiwezi kutikiswa kwa namna yoyote na Vyama vilivyoundwa Mwaka 1992 huku vyama hivyo vikidhani vimeshapata mbavu na uwezo wa kuongoza nchi.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Leave a Comment