×

Ndejembi Aitaka Tantrade Kutafuta Masoko Zaidi ya Kimataifa Kwa Bidhaa za Tanzania

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuongeza juhudi za kutafuta na kupanua masoko ya kimataifa kwa bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuongeza fursa za biashara na kukuza mauzo ya nje.

Ndejembi amesema TANTRADE inapaswa kufanya tafiti za kina kuhusu bidhaa zinazohitajika katika masoko ya kimataifa pamoja na kubaini viwango vya ubora vinavyotakiwa ili kuwawezesha wazalishaji wa Tanzania kuandaa bidhaa zinazokidhi mahitaji ya wanunuzi wa nje.

Amesema kufanya hivyo kutasaidia bidhaa za Tanzania kuwa na ushindani katika soko la kimataifa, kuongeza idadi ya wanunuzi na kufungua fursa zaidi kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa ndani.

Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo wakati akitembelea mabanda mbalimbali katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, yanayofanyika katika viwanja vya TGT mkoani Arusha, kabla ya ufunguzi rasmi wa maonesho hayo.

Katika ziara hiyo, alipata fursa ya kujionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wadau wa sekta ya kilimo cha bustani pamoja na shughuli zinazofanyika katika kukuza biashara na uwekezaji katika sekta hiyo.

Maelekezo hayo yanaweka msisitizo katika umuhimu wa kuunganisha wazalishaji wa ndani na masoko ya kimataifa, huku sekta ya kilimo cha bustani ikiendelea kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa za kuongeza thamani ya mazao na kukuza biashara ya Tanzania.

Leave a Comment