×

Heche Afunguka Kuhusu Maridhiano, Asema Chadema Haijakataa Mazungumzo

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, amesema chama hicho hakijawahi kukataa maridhiano, bali kinahitaji mazungumzo ya kweli yatakayofanyika kwa uwazi, bila hila wala udanganyifu, ili kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa nchini.

Heche ameyasema hayo leo Novemba 10, 2026, alipokuwa akizungumza katika msiba wa kaka wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, wilayani Ikungi, mkoani Singida.

Amesema CHADEMA iko tayari kushiriki katika mazungumzo yatakayolenga kurejesha hali ya kisiasa nchini, lakini amesisitiza kuwa chama hicho hakitashiriki mazungumzo hayo wakati Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, akiwa gerezani.

Kwa mujibu wa Heche, Lissu ndiye anayepaswa kuongoza mazungumzo hayo kwa upande wa chama hicho, akieleza kuwa uwepo wake ni muhimu katika kutafuta suluhu ya changamoto za kisiasa zinazokabili nchi.

Aidha, Heche ametoa wito wa kuachiliwa huru kwa Lissu, akisisitiza kuwa kwa mtazamo wake hana hatia wala kosa linalopaswa kumfanya aendelee kubaki gerezani.

Ameongeza kuwa maridhiano ya kweli hayawezi kujengwa kwa kauli pekee, bali yanahitaji uwazi, ukweli na haki kutoka kwa pande zote zinazohusika.

Kauli hiyo ya Heche inaweka wazi msimamo wa CHADEMA kuhusu masharti wanayoyataka yazingatiwe kabla ya kushiriki mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa nchini.

Leave a Comment