
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amevitaka vikundi vya ulinzi shirikishi vya Sungusungu nchini kutowatenga wananchi kutokana na imani zao za kidini wala kuwalazimisha kushiriki taratibu zinazokinzana na misingi ya imani zao, akionya kuwa vitendo hivyo vinaweza kusababisha migawanyiko katika jamii.
Dkt. Mwigulu alitoa maelekezo hayo Jumanne, Novemba 10, 2026, wakati akisikiliza kero na malalamiko ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Singita, Kata ya Usanda, Jimbo la Itwangi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Alisema ni muhimu kuheshimu uhuru wa wananchi kuabudu kwa kufuata imani zao, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu anayepaswa kulazimishwa kufanya jambo linalokwenda kinyume na dhamiri yake.
“Kama mtu imani yake haimruhusu kuchanja, kwa kweli tusimlazimishe. Na wala tusimtenge,” alisema Waziri Mkuu.
Kauli hiyo ilifuatia malalamiko yaliyowasilishwa na mwananchi Simon John, aliyedai kuwa mchungaji wake ametengwa na baadhi ya wanajamii baada ya kukataa kushiriki taratibu fulani za Sungusungu, hali iliyosababisha hata waumini wake kuzuiwa kwenda kusali katika kanisa lake.

Akijibu malalamiko hayo, Dkt. Mwigulu alizungumza na kiongozi wa Sungusungu aliyekuwepo katika mkutano huo na kumtaka kuhakikisha mchungaji huyo hapati usumbufu, anaheshimiwa na anaendelea kupata ulinzi.
“Msisumbuane na mchungaji mmoja huyo. Mpeni na ulinzi, wala msimtenge,” alisisitiza.
Aidha, aliielekeza Sungusungu kuhakikisha wananchi wote, wakiwemo wanachama wa vikundi hivyo, wanakuwa huru kwenda kusali kwa mchungaji huyo bila kuzuiwa, akisisitiza kuwa tofauti za kiimani hazipaswi kuwa chanzo cha migogoro katika jamii.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliahidi kuchukua hatua kuhusu ajira za walimu wawili waliojitolea kufundisha katika Shule ya Msingi Masunula kwa zaidi ya miaka mitano.
Alisema atamwandikia Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ili walimu hao wazingatiwe katika mchakato wa ajira kutokana na mchango wao katika kuinua kiwango cha ufaulu shuleni hapo.
Walimu hao wameelezwa kuchangia mafanikio ya Shule ya Msingi Masunula kushika nafasi ya pili kitaifa, jambo lililoibua hatua ya Waziri Mkuu kutaka mchango wao utambuliwe.
Maelekezo hayo yanaweka msisitizo katika kuheshimu uhuru wa dini na ibada, kuimarisha mshikamano wa wananchi na kutambua mchango wa walimu katika kuboresha elimu nchini.
