
ANTALYA, UTURUKI: Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ameitaka jumuiya ya kimataifa kuweka utaratibu wa kutathmini na kutoa fidia kwa uharibifu wa mazingira uliosababishwa na mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel dhidi ya nchi hiyo.
Pezeshkian ametoa kauli hiyo Jumatano, Novemba 11, 2026, wakati akihutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP31) unaofanyika mjini Antalya, Uturuki.
Amesema kuna umuhimu wa kuweka uhusiano wa moja kwa moja kati ya ahadi za nchi katika kulinda mazingira wakati wa amani na wajibu wa kuwajibika pale mazingira yanapoharibiwa wakati wa vita.
Iran inataka jumuiya ya kimataifa kuanzisha mifumo ya kurekodi, kutathmini na kuweka utaratibu wa fidia kwa madhara ya kimazingira yanayotokana na mashambulizi ya kijeshi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashambulizi katika mzozo wa Iran, Marekani na Israel yamehusisha miundombinu ya nishati, huku pia kukiwa na mashambulizi dhidi ya meli katika eneo la Ghuba na njia muhimu ya bahari ya Hormuz.
Mashambulizi hayo yamesababisha madhara ya kimazingira, yakiwemo kumwagika kwa mafuta baharini na uchafuzi unaotokana na kuharibiwa kwa miundombinu ya nishati.
Hata hivyo, mikataba ya sasa ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi haina utaratibu maalumu wa kutoa fidia kwa uharibifu wa mazingira unaosababishwa na mashambulizi ya kijeshi.
Kwa sasa, mifumo ya ufadhili wa tabianchi inalenga zaidi kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kugharamia hatua za kukabiliana na madhara yake.
Wakati huohuo, ripoti ya muungano wa wanasayansi wa kimataifa iliyotolewa Jumanne imeeleza kuwa uzalishaji wa hewa chafu duniani unatarajiwa kupungua kidogo mwaka huu, hali ambayo kwa sehemu imehusishwa na kupanda kwa bei za nishati kutokana na vita na kuongezeka kwa matumizi ya nishati jadidifu.
Kauli ya Iran imefungua mjadala mpana kuhusu uwajibikaji wa kimataifa katika kulinda mazingira wakati wa migogoro ya kijeshi na uwezekano wa kuanzishwa kwa mfumo maalumu wa fidia kwa nchi na jamii zinazokumbwa na athari hizo.