×

CAF Kutumia VAR Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika

CAIRO, MISRI: Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kupitia Rais wake Dkt. Patrice Motsepe, limetangaza kuanza kutumika rasmi kwa teknolojia ya Usaidizi wa Mwamuzi wa Video (VAR) kuanzia hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Uamuzi huo unaweka historia mpya katika soka la klabu barani Afrika, kwani kwa mara ya kwanza teknolojia hiyo itatumika kuanzia hatua ya makundi badala ya kusubiri hatua za robo fainali au hatua za mwisho za mashindano.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, matumizi ya VAR yataanza baada ya kumalizika kwa mapumziko ya kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Hatua hiyo inalenga kuongeza usahihi wa maamuzi ya waamuzi, kupunguza makosa yanayoweza kuathiri matokeo ya michezo pamoja na kupunguza malalamiko kutoka kwa timu zinazoshiriki mashindano hayo.

Teknolojia ya VAR hutumika kuwasaidia waamuzi kupitia upya matukio muhimu ya mchezo, yakiwemo mabao, maamuzi ya penalti, kadi nyekundu za moja kwa moja na makosa ya utambulisho wa wachezaji.

Uamuzi wa CAF unatarajiwa kuongeza uwazi na kuimarisha ushindani wa haki katika mashindano makubwa ya klabu barani Afrika.

Hata hivyo, matumizi ya teknolojia hiyo hayamaanishi kuwa malalamiko yote kuhusu maamuzi ya waamuzi yataisha, kwani VAR bado hutegemea tafsiri ya sheria za mchezo na maamuzi ya mwisho ya mwamuzi wa uwanjani.

Leave a Comment