
Zanzibar imepokea ugeni wa kipekee baada ya mshindi wa taji la Miss World 2026, Joheirry Molla, kuwasili visiwani humo Novemba 19, 2026, akiwa ameambatana na warembo kutoka mabara sita duniani.
Ziara hiyo ni sehemu ya safari yake nchini Tanzania inayolenga kutangaza vivutio vya utalii, utamaduni na uzuri wa maeneo mbalimbali ya nchi, huku ikitoa hamasa kuelekea mashindano ya Miss World 2027 yanayotarajiwa kufanyika Tanzania.
Akiwa Zanzibar, Miss Molla anatarajiwa kutembelea hoteli na maeneo mbalimbali ya utalii ambayo yanatajwa kuwa sehemu ya maandalizi ya mashindano hayo.

Akizungumza baada ya kuwasili, Joheirry Molla amesema amevutiwa na utamaduni wa Tanzania pamoja na mapokezi mazuri aliyoyapata, huku akieleza kuwa ana hamu ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Zanzibar na kujionea uzuri wake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Emmanuel Ishengoma, amesema Serikali inalenga kutumia fursa ya kuandaa mashindano ya Miss World kukuza uchumi, kuimarisha sekta ya utalii na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Ziara hiyo inaweka Zanzibar katika nafasi ya kuonyesha utajiri wake wa utamaduni, historia na vivutio vya utalii kwa wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.







