×

Mbunge wa Adai AI Kutumika Kupanga Mashambulizi ya Kigaidi

Mbunge wa Marekani kutoka chama cha Republican, Chip Roy.

Mbunge wa Marekani kutoka chama cha Republican, Chip Roy, ameitaka serikali ya nchi hiyo kuweka hatua kali zaidi za kisheria dhidi ya watu wanaosaidia mataifa yanayoonekana kuwa maadui wa Marekani kutumia teknolojia za kisasa, hususan akili mnemba (AI), kwa shughuli zinazoweza kuhatarisha usalama wa taifa.

Roy ametoa kauli hiyo katika mahojiano na kituo cha Newsmax siku ya Alhamisi, akieleza kuwa maendeleo ya kasi ya teknolojia ya AI yameongeza changamoto mpya za kiusalama ambazo zinahitaji serikali na Bunge la Marekani kuchukua hatua za haraka.

Onyo lake limekuja baada ya ripoti ya serikali kuonesha kuwa wachunguzi waliweza kukwepa mifumo ya ulinzi ya majukwaa manne makubwa ya AI, ambayo ni ChatGPT, Claude, Grok na Gemini, na kuyatumia kupata maelekezo ya kina kuhusu namna ya kupanga mashambulizi ya kigaidi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wachunguzi waliweza kupata maelekezo yanayohusiana na matumizi ya vilipuzi, mashambulizi dhidi ya miundombinu ya umeme na matukio mengine yanayoweza kusababisha vifo vya watu wengi ndani ya kipindi kisichozidi saa 12.

Akizungumzia hali hiyo, Roy amesema teknolojia ya AI inabadilika kwa kasi kubwa na kwamba Marekani inahitaji kuweka mifumo imara ya ulinzi ili kuzuia matumizi yake yanayoweza kuhatarisha usalama wa taifa.

Amesisitiza kuwa serikali inapaswa kuimarisha udhibiti wa teknolojia nyeti bila kuathiri haki za kikatiba za raia wa Marekani.

Aonya kuhusu teknolojia ya Marekani kuuzwa China

Katika mahojiano hayo, Roy pia amezikosoa kampuni za teknolojia za Marekani kwa kuuza vifaa vya kisasa vya kutengeneza semikondakta kwa China, akionya kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kuimarisha uwezo wa kiteknolojia wa taifa hilo katika maeneo yanayoweza kuleta changamoto kwa usalama wa Marekani.

Amesema maslahi ya kibiashara hayapaswi kupewa kipaumbele kuliko masuala ya usalama wa taifa, akidai kuwa Marekani imekuwa ikichangia kuimarisha uwezo wa mataifa yanayoweza kushindana nayo.

Mbunge huyo pia ameeleza wasiwasi kuhusu uwezekano wa mataifa ya kigeni kupata taarifa nyeti kupitia ushirikiano na vyuo vikuu pamoja na taasisi za utafiti nchini Marekani.

Amezitaja China na Qatar katika kueleza wasiwasi wake kuhusu ushawishi wa mataifa ya nje katika taasisi za elimu na utafiti, ikiwemo zile zinazohusika na miradi ya ulinzi wa taifa.

Roy amesema ajenda ya Rais Donald Trump ya ‘America First’ inapaswa kuzingatia kulinda uwezo wa Marekani katika teknolojia na masuala ya kijeshi ili kuendelea kuwa na nafasi ya kimkakati duniani.

Ameonya kuwa kushindwa kulinda ubora wa kiteknolojia wa Marekani kunaweza kudhoofisha uwezo wa nchi hiyo kujilinda dhidi ya vitisho vya baadaye.

Leave a Comment