×

Rais Samia Kufungua Mkutano wa Wakuu wa Tume za Uchaguzi za SADC Dar, Novemba 23, 2026

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi  Ramadhani Kailima.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 28 wa Mwaka wa Tume za Uchaguzi za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (ECF-SADC), utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 23, 2026.

Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kukutanisha viongozi na watendaji wakuu wa taasisi za usimamizi wa uchaguzi kutoka nchi 15 wanachama wa jumuiya hiyo, wakiwemo wenyeviti wa tume za uchaguzi, makamishna na maofisa waandamizi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima, amesema mkutano huo utatoa fursa kwa nchi wanachama kukutana na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa chaguzi katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Amezitaja nchi zitakazoshiriki kuwa ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Eswatini, Lesotho, Malawi na Mauritius.

Nyingine ni Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Shelisheli, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano huo kupitia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), huku Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) nayo ikiwa miongoni mwa taasisi zitakazoshiriki.

Mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha wadau wa usimamizi wa uchaguzi kutoka mataifa mbalimbali ya ukanda huo kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kujadili masuala yanayohusu taasisi za uchaguzi katika nchi wanachama wa SADC.

Kufanyika kwa mkutano huo jijini Dar es Salaam kunaifanya Tanzania kuwa kitovu cha majadiliano ya kikanda kuhusu masuala ya uchaguzi kwa siku hizo mbili.

Leave a Comment