×

Wagombea Watano Wajitokeza Kugombea Uenyekiti Simba

Uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC umeanza kupata ushindani baada ya wanachama watano kujitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi hiyo ya uongozi ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa waliojitokeza ni Swedy Mkwabi, Geoffrey Nyange Kaburu, Dkt. Seif Muba na Mohammed Soloka, ambao wamechukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi hiyo, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mwandishi wa habari Nassib Mkomwa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii.

Jina jingine lililojitokeza ni Mwenyekiti wa sasa wa Simba, Murtaza Mangungu, ambaye pia amechukua na kurejesha fomu ya kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine. Taarifa zinaeleza kuwa Mangungu alichukua fomu hiyo majira ya saa sita mchana na kuirejesha saa tisa alasiri.

Kujitokeza kwa majina hayo kunaashiria ushindani katika mchakato wa kuwania nafasi ya mwenyekiti wa klabu hiyo, huku wanachama hao wakionesha nia ya kuongoza moja ya klabu kubwa za soka nchini Tanzania.

Hata hivyo, mchakato wa uchaguzi utaendelea kufuata taratibu na kanuni za uchaguzi za klabu, kabla ya kupatikana kwa wagombea watakaokidhi vigezo na hatimaye mwanachama atakayepata ridhaa ya kuiongoza Simba SC.

Leave a Comment