MOSHI, KILIMANJARO: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuunda Tume ya Maridhiano ya Kitaifa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kurejesha mshikamano, kuimarisha umoja wa Taifa na kuweka msingi wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba.

Rais Samia ameyasema hayo leo, Novemba 20, 2026, katika Shule ya Polisi (CCP), Moshi mkoani Kilimanjaro, wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maofisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi wenye kaulimbiu isemayo “Usalama Endelevu ni Msingi wa Dira ya Taifa ya 2050.”

Amesema Serikali imeanza mashauriano na makundi mbalimbali ya kijamii, yakiwemo viongozi wa dini, vyama vya siasa na taasisi za kiraia, kwa lengo la kupata wawakilishi watakaoshiriki katika Tume hiyo, ambayo inatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
Amesisitiza kuwa Tume hiyo itakuwa na jukumu la kusaidia kulirudisha Taifa pamoja, kutambua hoja na changamoto zinazowakabili wananchi, pamoja na kujadili maeneo yanayohitaji mabadiliko katika Katiba.

Akizungumzia matarajio ya mchakato wa Katiba, Rais Samia amesema Serikali inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2028 au 2029 nchi inakuwa imepiga hatua katika kupata Katiba iliyorekebishwa au Katiba Mpya.
“Kama tulivyoahidi kwenye Ilani, tukifika 2028, 2029 tayari tutakuwa na Katiba iliyorekebishwa, au jina lolote mnalopenda kuiita, Katiba Mpya, Katiba iliyorekebishwa, tutakuwa tayari tuko nayo mikononi,” amesema Rais Samia.

Ameeleza kuwa wazo la kuunda Tume ya Maridhiano limetokana na mapendekezo ya Tume iliyochunguza matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambayo yalihusisha changamoto za kiusalama nchini.
Katika eneo la usalama, Rais Samia amelipongeza Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa juhudi za kulinda amani na utulivu wa nchi, akisema hali ya usalama imeendelea kurejea katika utulivu licha ya changamoto zilizojitokeza mwaka 2025.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Tume iliyochunguza matukio hayo, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga mazingira yatakayowezesha wananchi kuwa na mshikamano na kushiriki katika masuala ya maendeleo ya Taifa.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema uchumi wa Tanzania unaendelea kukua na kwamba nchi hiyo inaongoza kwa ukuaji wa uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia sita mwaka 2025 na unatarajiwa kukua kwa kati ya asilimia 6.3 na 6.5 mwaka 2026.
Ameeleza kuwa ukuaji huo hauonekani katika takwimu na nyaraka za Serikali pekee, bali pia katika shughuli za kiuchumi za wananchi, akibainisha kuwa wananchi wanaendelea kufanya biashara na kumiliki fedha kutokana na shughuli mbalimbali za uzalishaji na biashara.

Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia usalama, kuimarisha uchumi na kutekeleza hatua zinazolenga kujenga umoja wa kitaifa, huku mchakato wa maridhiano ukitarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya mabadiliko ya Katiba nchini.