

DAR ES SALAAM, Novemba 27, 2026 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaapisha mawaziri watano katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Novemba 27, 2026.
Mawaziri walioapishwa ni pamoja na Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na Balozi Mahmoud Thabit Kombo, aliyeapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
wengine walioapishwa ni Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Waziri wa Mifugo, David Ernest Silinde, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na Beng’i Mazana Issa, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Uapisho huo umefanyika siku mbili baada ya Rais Samia kutangaza mabadiliko ya muundo wa baadhi ya wizara, uteuzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali serikalini, hatua iliyohusisha pia kugawanywa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Katika mabadiliko hayo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imegawanywa na kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Vilevile, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imegawanywa na kuunda Wizara ya Mifugo na Wizara ya Uvuvi, huku Hamis Mohamed Mwinjuma akiteuliwa kuwa Waziri wa Uvuvi.


