
DAR ES SALAAM – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya nchini kutekeleza ipasavyo majukumu yao ya kuwahudumia wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili badala ya kumwachia Waziri Mkuu jukumu hilo.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo, Novemba 27, 2026, wakati akizungumza katika hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Amesema si sahihi kwa viongozi wa ngazi za mikoa na wilaya kushindwa kushughulikia kero za wananchi katika maeneo yao na kumwachia Waziri Mkuu kuzunguka nchi nzima kusikiliza na kutatua changamoto ambazo zingeweza kumalizwa na viongozi hao.
Ameeleza kutoridhishwa kwake na mwenendo wa baadhi ya viongozi hao, akibainisha kuwa migogoro midogo ya ardhi na mashamba inapaswa kushughulikiwa katika ngazi husika badala ya kusubiri Waziri Mkuu aingilie kati.

“Kazi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya ni kwenda kule kwa wananchi kujua shida zao, hiyo kazi sio ya Waziri Mkuu. Mpumzisheni, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya waende wakafanye kazi yao, lakini Waziri Mkuu ndio anazunguka,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amemtaka Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Eliakim Maswi, kuhakikisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kusimamia uwajibikaji wa watumishi wa umma katika maeneo yao.

Amesisitiza kuwa viongozi hao wanapaswa kuwa karibu na wananchi, kusikiliza kero zao na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi bila kuchelewa.
Amesema utekelezaji wa majukumu hayo utasaidia kumpunguzia Waziri Mkuu mzigo wa kushughulikia changamoto za ngazi za chini na kumpa nafasi ya kuzingatia jukumu lake kuu la kuratibu shughuli za Serikali.
Maelekezo hayo yanakuja wakati Serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa viongozi na watumishi wa umma katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na changamoto zao zinatatuliwa kwa wakati.