
DAR ES SALAAM – Wapiganaji wa mchezo wa mapigano wa Mixed Martial Arts (MMA), Christ Benda na Rashid “Nyundo” Mlegelo, wameendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kupitia mashindano ya kimataifa, wakionyesha dhamira, nidhamu na uwezo wa vijana wa Kitanzania katika mchezo huo.
Wakizungumza katika mahojiano maalumu, wapiganaji hao wameeleza safari zao katika mchezo wa MMA, maandalizi yao ya kila siku pamoja na umuhimu wa kuiwakilisha Tanzania kila wanapopanda ulingoni.
Christ Benda, anayeshiriki katika uzito wa Flyweight, ana rekodi ya ushindi mara tatu na kupoteza pambano moja (3-1). Amesema safari yake imejengwa katika mazoezi, kujituma na nidhamu, akifanya maandalizi yake katika vituo vya MMA Dar na Fight Academy Tanzania.
Benda anatarajiwa kurejea ulingoni Desemba 5 kupitia mashindano ya ANZA MMA, katika pambano linalokuja wakati Tanzania ikijiandaa kuadhimisha miaka 65 ya Uhuru.
Kwa upande wake, Rashid “Nyundo” Mlegelo naye ameendelea kuonyesha uwezo mkubwa ndani ya mchezo huo, baada ya kupata tuzo ya Submission of the Night katika mashindano ya ANZA MMA Pro Night 002 na ushindi wa Technical Knockout (TKO) katika Pro Nights 3.
Mlegelo amesema mazoezi na maandalizi katika MMA Dar na Fight Academy Tanzania ni sehemu muhimu ya safari yake ya kujiimarisha na kuendelea kufanya vizuri katika mashindano.

Mafanikio ya wapiganaji hao yanaongeza hamasa kwa vijana wanaopenda michezo ya mapigano nchini, huku yakionyesha nafasi ya MMA katika kuitangaza Tanzania kupitia vipaji vya wanamichezo wake.
Wakati taifa likielekea kutimiza miaka 65 ya Uhuru, Christ Benda na Rashid “Nyundo” Mlegelo ni miongoni mwa wanamichezo wanaobeba matumaini ya kuendeleza jina la Tanzania katika medani ya MMA.
Desemba 5, macho na matumaini ya mashabiki wa MMA Tanzania yatakuwa kwa Christ Benda anaporejea tena ulingoni katika mashindano ya ANZA MMA.