
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka wahitimu wa vyuo vikuu nchini kutumia elimu na ujuzi walioupata kuanzisha shughuli za kiuchumi na kubuni njia za kutatua changamoto mbalimbali za jamii badala ya kutegemea ajira pekee.
Amesema mabadiliko katika soko la ajira yanawahitaji wahitimu kuwa wabunifu, kujiamini na kuthubutu kutekeleza mawazo yao, badala ya kukata tamaa wanapokabiliwa na changamoto.

Dkt. Mwigulu ametoa rai hiyo leo (Jumamosi, Novemba 28, 2026) wakati akihutubia Mahafali ya 12 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo, Tabora (AMUCTA), yaliyofanyika mkoani Tabora.
Amesema tofauti na miaka ya nyuma, ambapo baadhi ya wanafunzi walikuwa wakipata nafasi za ajira kabla hata ya kuhitimu masomo, hivi sasa idadi ya wahitimu imeongezeka na ushindani katika soko la ajira umekuwa mkubwa.

Amesisitiza kuwa hali hiyo haipaswi kuwakatisha tamaa vijana, bali iwahimize kutumia maarifa na ujuzi wao kujitengenezea fursa za kiuchumi na kushiriki katika kutatua changamoto zinazokabili jamii.
Amewataka wahitimu kutoruhusu hofu au kukata tamaa kuwazuia kutekeleza mawazo yao ya ubunifu kabla hata ya kuyajaribu, akisema wanapaswa kuwa na uthubutu na uvumilivu katika kufikia malengo yao.

Waziri Mkuu pia amewataka wahitimu kuondokana na mtazamo wa kujidharau au kuamini kwamba hawawezi kupata ajira bila kuwa na watu wanaowafahamu katika taasisi zinazotoa nafasi za kazi.
“Nataka kila mmoja wenu ajiamini. Ukijikadiria kadirio la chini wewe mwenyewe, mwingine akikutazama hakuoni. Jiamini,” amesema.

Akielezea uzoefu wake, Dkt. Mwigulu amesema aliwahi kuomba nafasi ya kazi ya mchumi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati akiwa bado hajakamilisha masomo yake ya shahada ya uzamili, licha ya tangazo la kazi hiyo kuhitaji mwombaji mwenye uzoefu wa angalau miaka mitatu.
Amesema aliamua kuomba nafasi hiyo na kufanya mtihani wa maandishi, ambapo alifaulu na kuitwa kwenye usaili wa ana kwa ana.
