×

Kilichojificha mgogoro wa Zanzibar -6

1963-un-zanzibarTunaendelea kuwasimulia kilichojifisha katika mgogoro wa kiasa Zanzibar.

Karume, ateta na Mwalimu
Katika mfululizo wa matangazo yake redioni Jumanne, Januari 14, 1964, John Okello, kama Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alitamka jambo la ajabu kwamba, mawaziri wa zamani wa Serikali ya ZNP/ZPPP wangenyongwa.
Jumatano, Januari 15, 1964, Abed Karume, alikanusha na kumpinga vikali kwamba, hakuna mtu atakayenyongwa, wala kulipiza kisasi. Huo ulikuwa mwanzo wa migongano kati ya viongozi hao wawili.
Alhamis, Januari 16, 1964, Rais Karume, Abdulrahman Babu na Kassim Hanga walikwenda Dar es Salaam kwa ndege kumuomba Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa rais wa Tanganyika  aitambue Serikali ya Mapinduzi pia asaidie kupeleka askari kurejesha utulivu.

Lakini kulikuwa na mengi nyuma ya maombi hayo.  Karume alikuwa ameingia katika mgogoro na viongozi wenzake wa ASP wenye siasa za kikomunisti, wakiongozwa na Othman Sharrif, wakidai alikuwa ameshindwa kuongoza, wakatishia kumpindua. Hawa waliungwa mkono na vijana wa ASP na Umma Party.
Ingawa Okello alijitahidi kusuluhisha mgogoro huo ukaonekana kumalizika, akaomba msaada wa ulinzi kutoka Serikali ya Tanganyika. Nyerere alikubali ombi hilo, baada ya siku mbili askari 300 walitumwa Zanzibar kurejesha kumlinda  Karume.

Miezi mitatu baadaye, Nyerere alishinikiza Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Awali Karume alionesha kutokuwa tayari kwa hilo, Mwalimu akatishia kuwaondoa askari wake ili kumwacha (Karume) akiwa hana wanajeshi, kitu ambacho kingekuwa hatari kwake  hivyo alisalimu amri na kukubali Muungano.

Siku hiyo Okello, pengine bila kujua safari ya Dar es Salaam ya Karume na wenzake na pengine kwa kuudhika na ubishi wake uliokuwa umeanza kujitokeza, alibatilisha uteuzi wa Karume kuwa rais, badala yake akamfanya Makamu wa Rais kwa madai kwamba hakushiriki hata kidogo katika kupigana wakati wa mapambano.
Jioni hiyo, Okello akajipa cheo cha rais. Lakini, pengine baada ya kushauriwa, alifuta mabadiliko hayo wakati tayari hatua hiyo ilikuwa imetia ufa wa kiuongozi kati yao.

Januari 16, 1964 mchana. Okello alifika Jumba la Makao Makuu yake Raha Leo,  akakuta mamia ya watu wamekusanyika wakimsubiri kwa shauku, wengi wamevaa vitambaa vya kijani. Alipojitokeza akiwa amevalia nguo nyeusi na bastola kiunoni, wananchi wakalipuka kwa shangwe wakisema kwa sauti: “Jamhuri!  Jamhuri!” Kila mmoja akiwania kumshika mkono.
Historia hii haifutiki licha ya wengine kutaka kuingiza udini.

Leave a Comment