×

Kilichojificha mgogoro wa Zanzibar -7

Tunaendelea kufafanua kuhusu mgogoro wa Zanzibar, endelea:

Jumapili 12, 1964 asubuhi, Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Nje wa Tanganyika, Oscar Kambona alikwenda Nairobi na Kampala na akiwa huko, akagundua kuwa Kenya na Uganda zilikuwa mbioni kuitambua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hivyo akaamua kumpigia simu Mwalimu Nyerere kumwomba naye afanye hivyo.

Jumatatu alasiri, Januari 13, 1964, Kenya na Uganda ziliitambua Serikali ya Okello; wakati huo Karume ndiyo kwanza alikuwa anarejea Zanzibar kutoka Dar es Salaam.

Kambona  alimjulisha Mwalimu Julius Nyerere juu ya sultani aliyepinduliwa kukataliwa kutia nanga Mombasa na Serikali ya Kenya na kumwomba naye amkatalie vivyo hivyo.

Nyerere aliyakataa maombi yote ya Kambona akidai kuwa, hakuwa na hakika kama kweli Karume na ASP walikuwa wameshika hatamu za uongozi visiwani; badala yake akamruhusu Sultani Jamshid na kikundi chake kutia nanga na kukaa Dar es Salaam.

Nimeeleza haya kuthibitisha kwamba, si Serikali ya Tanganyika, wala jumuiya kubwa ya Kizanzibari, iliyoamini kwamba Mapinduzi hayo yalisimamiwa na viongozi wakuu wa ASP; bali kwamba yalifanywa na vijana wa ASP na Umma Party bila matarajio wala viongozi wao kujua.

Januari 13, 1964, Kiongozi wa mapinduzi hayo, ambaye awali alijitambulisha kwa cheo tu cha “Field Marshal”, alijitambulisha kikamilifu redioni kwa jina la Field Marshal John Okello kisha akasema: “Sultani amefukuzwa na hatakanyaga tena ardhi ya Zanzibar; jumba lake na mali zake zimetaifishwa.”
Baadaye  Okello akaomba kutoka  Serikali ya Tanganyika shehena ya ndege nzima ya dawa na akatoa amri kwa madaktari na wauguzi wote kurejea kazini jioni hiyo.

Katika kuhakikisha usalama wa mali za raia na juu ya vitendo vya usaliti, Okello alionya:  “Mtu yeyote atakayejaribu kuwa mnafiki, atapata adhabu ya kifungo cha miaka hamsini; atakayeiba, hata mche wa sabuni,
ataadhibiwa kifungo cha miaka minane. Mimi naweza kutengeneza mabomu mia nane kwa saa moja”
Siku nyingine, katika kuonesha kwamba alikuwa kiongozi mwenye mamlaka ya kijeshi alisema:  “Mimi ni Field Marshal ninayezungumza. Mtaona jinsi tunavyowanyonga watu na kuwachoma kama kuku.  Wengine watakatwa vipandevipande na kutandazwa mitaani; wengine watatupwa baharini na wengine watafungwa kwenye miti na kupigwa risasi.”
Itaendelea wiki ijayo

Leave a Comment