NCHI inatikisika, kila idara ya serikali inaguswa na hakuna mtu aliyejihakikishia kuwa yupo salama hasa kama ameboronga, awe mkubwa, wa kati au mdogo, ilimradi yeyote anayekwenda kinyume na taratibu, siku zake zinahesabika.
Serikali sasa imerejesha heshima, angalau mtu akiambiwa serikali imesema, anashtuka, anajua wenye nchi yao wanaongea na kwa hakika wanaongea kwa mamlaka waliyopewa.
Ingawa bado ni mapema sana kuweza kuona unafuu wa maisha ya wananchi wa kada ya chini, lakini kuna dalili kwamba baada ya mwaka mmoja au miwili, joto linalokaba hali mbaya ya maisha, litaanza kupungua kama siyo kumalizika kabisa.
Hata hivyo, kuna baadhi ya mambo yanayofanyika yanaenda ndivyo sivyo, hayafanani na ahadi tulizopewa wakati wa kampeni au hata kabla ya hapo na viongozi wetu. Mfano hai ni matarajio ya wananchi kuhusu gesi asilia, inayotoka Mtwara.
Tuliambiwa, pamoja na kupata umeme kwa bei nafuu kwa watumiaji wa kawaida, bado hata baadhi ya bidhaa, zinazozalishwa kwa kutumia nishati hiyo, nazo zitapungua bei, mojawapo ikiwa ni saruji.
Tuna viwanda vingi vya bidhaa hii, lakini kupitia nishati hiyo, tukaahidiwa bei yake itapungua, kwani gharama za uzalishaji kwa viwanda hivyo itashuka sana.
Leo hii, pamoja na ongezeko la viwanda, hali imekuwa ni tofauti kabisa. Wananchi wa Mtwara, ambao walipaswa kunufaika na bei za vitu vinavyotokana na gesi asilia, bado hawajanufaika. Bei ya saruji haifahamiki hadi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipohoji bei hasa ya saruji hiyo.
Kinachoonekana, hawa wenye viwanda wamekaa na kukubaliana bei, bila kujali gharama za uzalishaji zilivyo. Licha ya viwanda kutumia gesi asilia, lakini wanauza bei utafikiri wanatumia mafuta.
Kama ambavyo serikali ilivyounda mamlaka zingine za kusimamia bei, huu ni wakati muafaka wa kuwa na chombo kinachosimamia bei ya bidhaa hii muhimu ili watu maskini wa nchi hii wapate uwezo wa kujenga makazi bora.
Watu wanajiuliza, hivi inawezekanaje saruji inayotengezwa nje ya nchi, kama Pakistan inauzwa hapa nyumbani kwa bei rahisi kuliko bidhaa iliyozalishwa ndani? Ni gharama gani kubwa wanayoingia wazalishaji wa ndani kama siyo ujanjaujanja wa kuwadhulumu wananchi?
Ni wakati muafaka sasa kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kutekeleza kwa vitendo ahadi yake ya kuondoa kero kwa wananchi. Gesi asilia inakuwa na maana zaidi kwa watu wa kipato cha chini kama bidhaa zitokanazo zinapatikana kwa bei rahisi.
Haina maana yoyote kama gesi hii itawasaidia wawekezaji kufanya vitu vyao kwa bei nafuu, halafu walaji wao, ambao ndiyo wananchi wetu, wakapata huduma hizo kwa bei kubwa.
Ushauri wangu ni kwamba iundwe mamlaka yenye uwezo kisheria wa kutoa bei elekezi kwa bidhaa hii ili kuwasaidia wananchi.
Nachochea tu!