×

Ajinyonga chumbani alikoenda kuiba

Na Paul Kayanda, RISASI mchanganyiko

KAHAMA: Mtu mmoja  ambaye hakufahamika jina lake mara moja, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 22-25 amefariki dunia kwa kujinyonga na shuka katika chumba cha mpangaji aliyejulikana kwa jina moja la Frank, mkazi wa Kata ya Malunga wilayani Kahama mkoani Shinyanga, alikovunja mlango na kuingia ndani kwa lengo la kuiba.

Afisa mtendaji wa Kata ya Malunga, Cosmas Bukango amesema tukio hilo lilitoka Aprili Mosi, majira ya saa 9.45 alasiri wakati mvua za masika zikiendelea kunyesha na watu wakiwa ndani, ndipo mtu huyo anayedhaniwa kuwa ni kibaka, alifika katika nyumba hiyo na kipande cha nondo kilichotumika kuvunja kufuli la mlango.

Bukango alisema wakati mtu huyo akivunja mlango na kuingia ndani kwa mpangaji huyo aliyekuwa kwenye mihangaiko ya maisha, jirani wa Frank, aitwaye Getruda Ziota alishuhudia zoezi zima, hivyo mara tu alipoingia, alinyata na kuufunga mlango wa chumba hicho kwa nje kabla ya kupiga kelele kuomba msaada.

Bukango alieleza kuwa baada ya kupewa taarifa hizo alifika katika eneo la tukio na kutoa taarifa kwa jeshi la Polisi Mjini Kahama. Inadaiwa wakati wananchi wakiwasubiri polisi, kibaka huyo aliamua kujihukumu, kwa kujinyonga kwa kutumia shuka aliyoifunga darini.

Akisimulia tukio hilo, Getruda Ziota alisema alikuwa ndani ya chumba chake akishona nguo wakati alipomuona mtu huyo akirandaranda, jambo lililomfanya ahisi ana lengo la kujikinga na mvua.

“Mvua ilipoanza kunyesha nilikaa ndani na kuanza kushona nguo, mara nikamuona mtu anakuja, akaingia chooni halafu akawa anachungulia kila sehemu, nikajua anajikinga mvua na kidogo nimuite aje ndani, roho ikasita, nikamuona anazidi kusogea chumbani, nikasimama juu ya stuli, nikamuona anatoa nondo na kubetua kufuli.”
Polisi waliuchukua mwili wa marehemu na hadi gazeti hili linaenda mitamboni, hakukuwa na taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu mtu huyo.

Leave a Comment