ILIPOISHIA GAZETI LA RISASI JUMATANO:
“Mpenzi…mpenzi…baba Rehema,” niliita lakini hakunisikiliza. Na mimi nikiwa kwenye kanga moja nikamfuata kwa nyuma, mbio, nikasikia paa..!
JIACHIE SASA…
“Haaa! Umeua baba Rehema jamani,” nilisema huku nikianza kulia nikiwa nafika sebuleni.
Kufika sebuleni, maana jumba lenyewe ni kubwa, sikumkuta mtu, nikatoka nikamkuta baba Rehema amesimama geti kubwa akiangalia nje huku akitukuna na kusema maneno mengine…
“Mna bahati sana nyie, ningemtegua mtu mguu. Mbuzi kasoro mkia nyie…yaone kwanza.”
Nilimshika mkono baba Rehema na kumrudisha ndani huku nikimbembeleza kwa kumwambia kwamba, aangalie mtoto. Anaweza kuua akajikuta anafungwa, je, Rehema atatunzwa na nani wakati mama yake ndiyo hivyo…
“Utamtunza hata wewe,” aliniambia.
Nilitamani maneno yake ayaandike kwenye karatasi ili yawe sehemu ya mirathi kwamba, yeye akiua, akifungwa mimi Jamila Katembo ndiyo nimlelee mtoto wake Rehema.
Nilitamani iwe hivyo kwa sababu nilijua ikitokea, nitakuwa namiliki lijumba lake likubwa na kujiachia kwa raha zangu. Hata wazazi wangu kijijini ningewaita kuja kuoga maji ya bomba la mvua.
Tuliingia ndani ambapo mimi nilifunga geti kwa kuloki, mtu wa nje asiweze kuingia bila ruhusa ya mtu wa ndani kufungua.
Tulifikia sebuleni, baba Rehema akasema…
“Leo siendi kazini, huyu mwanamke ameniharibia siku sana,” alisema baba Rehema…
“Hata mimi nakubali mume wangu, amekuharibia siku kweli. Anachokufanyia sasa ni udhalilishaji. Huenda ulitaka kumsamehe lakini kwa mwenendo wake huu inakuwa kazi sana, hata ningekuwa mimi,” nilisema nikijifanya niko kati kwa kati lakini kumbe maneno yangu yalijaa upepo wa moto…
“Si umeona, simsamehi tena yule mwanamke,” aliwaka baba Rehema…
“Nakuunga mkono lo! Kukuletea watu hapa nyumbani eti amekufumania ni kukosa adabu. Angefanya hivi kwa mwanaume wa hivyohivyo lakini si wewe mtu na heshima zako bwana…”
“Umeona ee?” alisema huku akipeleka mkono wake kwenye bega langu la kulia maana mimi nilikuwa kushoto kwake.
Nikamwona anashika simu na kubonyeza namba, nikajua anampigia mama Rehema. Mimi kimya, nikawa namwangalia tu huku nikisemea moyoni…
“Si umpe talaka tu.”
“Wee mama Rehema nataka kukwambia kwamba, kama unataka kukutana na kinu cha kutwangia kokoto basi ni mimi. Niogope sana. Tafuta mwingine wa kupambana naye…”
“Mpe… mpe… mpe tena,” mimi nilishadadia kwa sauti huku nikimshikashika baba Rehema kwenye tumbo lake lenye mafuta na kumfanya kuwa na kitambi cha kiaina…
“Niache kama nilivyo. We si umeamua kuwa na huyo mnuka kojo endelea naye. Msichana gani hajui hata kuoga, hajui rangi ya midogo inapakwa wapi. Akitembea kama anarudi kinyumenyume…
“Hayo magauni yenyewe anayovaa utadhani yametundikwa sokoni Karume. Ukimwita akufuate anavyokuja utasema ndiyo anaondoka kwenda mbele…”
Niliachia kicheko mwenzenu. Angekuwa mwingine najua angekasirika, ila mimi nilicheka kwa sababu sifa hizo zote ni zake sasa sikujua ni kwa nini aliamua kujimaliza mwenyewe.
Huyu mwanamke mama Rehema akisimama mbele yako akakupa bega, ukimwangalia unaweza kusema anakoangalia ndiyo nyuma maana ana tumbo kubwa na ana wowowo sasa hujui wapi mbele.
Mara nyingi sura yake iko kama amelamba maji yenye ndimu. Mimi sijawahi kumwona akicheka, labda siku moja tu napo niligundua kuwa, alilewa.
Unene wake ulivyo, huwezi kujua kiuno kiko sehemu gani maana akianza juu ni mpaka chini. Mzimamzima. Sasa kuona leo ananimwagia mimi sifa ambayo sina, namshangaa sana…
“Mama Rehema…mama Rehema,” aliita baba Rehema baada ya kugundua hana mpango wa kukatisha kuongea akinichana mimi…
“Tena huyo malaya atakuletea Ukimwi, mimi nipo hapa…”
“Mama Rehema naongea na wewe…unadhani wewe na Jamila nani ambaye anaweza kuleta Ukimwi hapa nyumbani?” baba Rehema alimuuliza kwa sauti iliyojaa ghadhabu ya hali ya juu kwa kiwango cha mwanaume…
“Jamila, mbona lipo wazi hilo?” mama Rehema alinipaka matope yake bila kujali atathari za mazungumzo hayo…
“Wewe umejisahau siyo unavyotembea na vitoto vidogovidogo na wewe limama lijitu lizima?” baba Rehema alimtupia kijembe…
Je, unajua nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi Jumatano ijayo.