ILIPOISHIA IJUMAA:
“Kwa nini nishindwe wakati ni kazi yangu? Mimi nafukuza jini hata akiwa mkubwa kama nyumba!”
“Sasa ameshanifanyia visa vingi sana na kutishia maisha yangu…”
“Usijali…usijali, mwisho wake ndiyo umefika. Wewe uje hii asubuhi nikushughulikie kabla watu hawajajaa.”
“Mengine nitakuja kukueleza hukohuko.”
“Sawa. Sasa unakuja?”
“Ninakuja. Nichukue shilingi ngapi?”
“Hiyo kazi ni kubwa lakini kwanza uje na shilingi laki tano.”
Pesa alizonitajia zilikuwa nyingi lakini kutokana na tatizo lililokuwa limenikabili nilimkubalia.
“Sawa, ninakuja sasa hivi.”
“Nakusubiri.”
Nikakata simu.
SASA ENDELEA…
Nilimfuata dada chumbani kwake, shemeji alikuwa ameshatoka kwenda kazini kwake.
Nikamueleza nilivyozungumza na yule mganga.
“Sasa hizo pesa unazo?” Dada akaniuliza.
“Pesa zipi?”
“Hizo alizotaka huyo mganga.”
“Nina nusu tu.”
“Sasa itakuwaje?”
“Niongezee laki mbili, mimi nitatoa laki tatu.”
“Kama pesa unazo si utoe tu, unafanya mchango wa nini?”
“Sina dada, nina shilingi laki tatu tu.”
“Kwani juzi huyo shetani wako si alikupa shilingi milioni kumi, ziko wapi?”
“Sitaki kutumia pesa zile.”
“Zina nini?”
“Zile tuziache kwanza.”
“Lakini si umeshaanza kuzitumia, sasa unaziacha kwa nini?”
“Dada naye ana maswali, wee nipe tu hizo laki mbili. Nitakuja kukurudishia.”
“Mimi sina laki mbili, labda nikupe laki moja halafu uirudishe.”
“Haya, nipe, nitairudisha.”
Dada akafungua kabati, akanitolea shilingi laki moja na kunipa.
“Hizo laki nne utaongezea mwenyewe.”
Sikumjibu, nilimuazima mkoba wake, nikazitia zile pesa.
“Basi mimi naenda.”
“Utakwenda na usafiri gani?”
“Nitachukua bodaboda.”
Nilipotoka nyumbani kwa dada, nilikodi bodaboda ambayo ilinipeleka nyumbani kwangu. Niliingia ndani. Nilikuwa nimeweka akiba yangu ya shilingi milioni moja. Nikachukua shilingi laki saba na kuacha laki tatu.
Nikabadili nguo nilizokuwa nimevaa kisha nikatoka. Nilipakiwa tena kwenye bodaboda, tukaanza safari ya kuelekea Tegeta kwa mganga.
Tulipofika Tegeta, nyumba na mtaa aliokuwa akiishi mganga huyo sikuvifahamu. Nikamwambia mwenye bodaboda asimame ili niwasiliane na mganga huyo.
Bodaboda iliposimama nikampigia simu mganga huyo na kumuuliza alikuwa anaishi mtaa gani? Akanielekeza mtaa na nyumba yake ilipokuwa. Hapakuwa mbali sana na pale tuliposimama.
Kwa vile sikutaka kijana huyo mwenye bodaboda ajue kuwa nilikuwa nakwenda kwa mganga, niliamua niende kwa miguu. Nikamlipa pesa alizotaka. Sasa nikawa navuka barabara. Ghafla nikaona teksi ikisimama mbele yangu.
Na mimi nikasimama na kuitazama. Katika siti ya nyuma niliona mtu mweupe akifungua mlango na kushuka.
“Mama yangu wee…!” Unadhani alikuwa nani?
Alikuwa ni yule Mzungu. Nilijikuta niko naye uso kwa uso.
“Hujambo Enjo?” akaniuliza kwa sauti tulivu huku akinitolea tabasamu la kihaini.
“Sijambo,” nikamjibu. Sauti yangu ilikuwa imefifia kwa hofu.
“Unakwenda wapi?”
Swali lake hilo lilinipa changamoto. Nikajiuliza nimwambie kuwa ninakwenda kwa mganga kwa ajili yake? Nisingethubutu. Nilitumia sekunde kadhaa kufikiria la kumjibu huku vitone vya jasho vikipamba kwenye paji la uso wangu.
“Hujui unakokwenda?” akaniuliza aliponiona nipo kimya.
Nikajidai kutabasamu ili asigundue kuwa nilikuwa nimegwaya lakini hata sikufanikiwa kulionesha hilo tabasamu. Tayari moyo wangu ulishafadhaika kukutana na shetani yule.
“Hapana. Ninakwenda nyumbani,” nikamdanganya.
“Ulikuwa unatoka wapi?”
“Ninatoka kule kumtembelea rafiki yangu.”
Nilimuonesha ule upande niliotokea.
Nafikiri aligundua kuwa nilikuwa namdanganya, akaufungua ule mlango wa nyuma wa gari na kuniambia.
“Ingia nikupeleke.”
Nikasita na kugeuza uso wangu upande mwingine.
“Ah! Nilikuwa nakwenda kukodi bodaboda…”
“Si umesema unakwenda nyumbani?” akaniuliza.
“Ndiyo nakwenda nyumbani.”
“Basi ingia tukupeleke, teksi ipo hapa.”
Pamoja na hofu niliyokuwa nayo, nilijikuta nikiingia kwenye ile teksi. Wakati najipakia ndipo liliponijia wazo kwamba ningekimbia badala ya kuingia kwenye teksi hiyo au ningepiga kelele kuita watu. Pengine ningefanya hivyo ningepata msaada.
Wazo hilo lilichelewa na lisingenisaidia kwa sababu nilikuwa nimeshajipakia kwenye ile teksi.
Yule M zungu naye akajipakia, tukawa tumekaa bega kwa bega.
Ujanja wangu wote kwisha!
Nikauinamisha uso wangu, nikaanza kusali kimoyomoyo huku nikijihisi nataka kulia.
Teksi ikaondoka. Hata sikujua ilikuwa inaelekea wapi. Mwili ulinifumka jasho ghafla. Nikajikuta ninatota kama ninayemwagiwa maji.
“Leo naenda kuuawa jamani!” nikawa najiambia kimoyomoyo.
“Kwa nini nimekubali kuingia kwenye hii teksi? Huyu jini ananipeleka wapi sasa?” nikawa najiuliza bila kupata jibu.
Teksi iliendelea kuyoyoma kuelekea mahali nisipopajua.
Je, nini kitaendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.
ee we enjo mwishowe dada ako nae atakuchoka na huyo shetani wako,ndo tujifunze wadada uroho wa hela we enjo c ulikuwa na mchumba huko ughaibuni ona sasa had kaka wa watu amekufa kusa uroho wako