Na Gladness Mallya
MMOJA wa waigizaji wakongwe katika tasnia ya filamu Tanzania ni Grace Mapunda ambaye ni maarufu kwa mashabiki kama Mama Kawele. Amefanya filamu nyingi na katika hizo, sehemu kubwa ameigiza kama mama, ambaye hata hivyo, nje ya kazi siyo mtu wa kuonekana sana, iwe katika magazeti au televisheni.
Gazeti hili lilifanikiwa kumfikia na kufanya naye mahojiano kuhusu mambo mbalimbali ya sanaa hiyo inavyoendelea.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo.
Swali: Mashabiki wako wangependa kujua umeanza lini sanaa na ilikuwa katika kundi gani?
Mama Kawele: Nilianza miaka 10 iliyopita katika kundi lililoitwa Splended lenye makao yake Ilala, Dar na baadaye nikahamia Shirikisho ambapo tulikuwa tukicheza michezo mbalimbali iliyokuwa ikirushwa kwenye Runinga ya ITV.
Swali: Ilikuchukua muda gani kufanya michezo ya televisheni kabla ya kugeukia katika filamu?
Mama Kawele: Nilifanya uigizaji kwenye vikundi kwa kiasi cha kama miaka minne hivi, lakini nikiwa Splended nilicheza filamu ya kwanza iliyojulikana kwa jina la Disukene.
Swali: Wewe binafsi una filamu ngapi hadi sasa?
Mama Kawele: Kiukweli sijawahi kucheza filamu yangu mwenyewe, huwa nashirikishwa tu za watu, lakini kabla ya mwakani nitacheza yangu.
Swali: Mpaka sasa umeshacheza filamu ngapi?
Mama Kawele: Yaani nimeshirikishwa kwenye filamu nyingi sana, hata sikumbuki idadi yake.
Swali: Ni kitu gani kilichokushawishi kuingia kwenye filamu?
Mama Kawele: Mwanangu wa kwanza ndiye aliyenishawishi kuingia kwenye sanaa, maana ndiye aliyeenda kunichukulia fomu nikajaza na kuanza kuigiza kwenye kikundi hicho cha Splended.
Swali: Vipi kuhusu familia yako?
Mama Kawele: Nina watoto wawili, lakini mume wangu alifariki miaka mingi iliyopita.
Swali: Ni mafanikio gani umeyapata kupitia kazi hii?
Mama Kawele: Mafanikio ni ya kawaida tu na ninamshukuru Mungu kwa hiki ninachokipata maana sanaa ni kazi yangu.
Swali: Mastaa, hasa wa filamu wamekuwa na skendo za ajabu kila kukicha, unafikiri ni kwa nini?
Mama Kawele: Sanaa ya sasa imevamiwa na watu wasio na vipaji, wengi wanaona ndiyo sehemu ya kukimbilia ili waweze kutimiza azma yao ya kuonekana na wanaume, hawana uchungu na sanaa.
Unajua wengi wao hawajapitia kwenye vikundi vya sanaa ili kujifunza maadili, wao wamevamia tu kwa vile wana muonekano mzuri basi, lengo la kuigiza kwao ni kutaka wapate mapedeshee.
Swali: Nini kifanyike ili kutokomeza tabia hizo?
Mama Kawele: Kwanza ninamshukuru Rais Magufuli kwa kutupa waziri mzuri mtendaji kazi, Nape Nnauye, serikali itusaidie kuwaondoa hawa wavamizi.
Swali: Unadhani waondolewe kwa staili gani?
Mama Kawele: Kuwe na vyuo maalum vya kujifunza sanaa na muigizaji ambaye hatapitia chuoni asiruhusiwe kufanya kazi hii. Pia ziwepo semina za kuwaelimisha wasanii, hii itasaidia kuwabadilisha wale waliovamia kwa lengo la kuuza sura tu na hawana vipaji ili waelewe kuwa hii ni kazi kama kazi zingine.
Swali: Ni kitu gani ambacho kinakukera katika maisha yako ya sanaa?
Mama Kawele: Huwa naumia sana pale mtu anaposhindwa kuheshimu kazi yangu na kuona ni uhuni, nataka watu watambue kuwa hii kwangu ni kazi kama nyingine jamani wasiidharau.
Swali: Tabia ya wasanii watu wazima kutoka kimapenzi na vijana wadogo unaizungumziaje?
Mama Kawele: Siwezi kukataa hayo yapo sana katika dunia ya leo, lakini niwaambie wanaofanya hivyo,
utakavyojiheshimu ndivyo utakavyoheshimiwa, siyo tabia nzuri kuwa na kijana anayeonekana kama mtoto wako kimapenzi.
Swali: Wasanii wa zamani wanalalamika kutoshirikishwa kwenye filamu hali inayosababisha maisha yao kuwa magumu, unafikiri ni kwa nini?
Mama Kawele: Siku hizi kujuana kwingi kuliko uwezo wa mtu, unakuta ‘scene’ inatakiwa mtu wa aina fulani, lakini mwenye filamu anamchukua ndugu au rafiki anamuweka.
Swali: Nini kinakosekana katika filamu baada ya kufariki kwa Steven Kanumba?
Mama Kawele: Kanumba alikuwa chachu, anajiamini na kujituma, lakini tuliobaki hatujiamini, hatuna uthubutu japokuwa kuna vijana wengi wanaofanya vizuri.
Swali: Nini siri ya kudumu kwenye tasnia kwa muda mrefu?
Mama Kawele: Siri ni kwamba ninaipenda, naithamini na kuiheshimu kazi yangu.
Swali: Unafanya kazi gani nyingine tofauti na filamu?
Mama Kawele: Filamu ndiyo kazi yangu kubwa, halafu nina biashara ndogondogo.
Swali: Mashabiki wangependa kujua baadhi ya filamu ulizocheza.
Mama Kawele: Zipo nyingi ila ninazozikumbuka ni Nifute Machozi, Jicho Langu, House Made na Tajiri Mtoto.
Swali: Unawaambia nini mastaa ambao ndoa zao zimevunjika na kuleta picha mbaya kwa wasanii?
Mama Kawele: Mpaka mtu unaamua kuolewa au kuoa umekubaliana na yote, sanaa na ndoa haviingiliani, wanatakiwa kupenda ndoa zao na kazi yao pia, wasiingie kwenye ndoa kwa ajili ya kuongeza tu idadi.
Swali: Nini tofauti ya sanaa ya zamani na sasa?
Mama Kawele: Sanaa ya zamani ilikuwa bora na nzuri, watu walikuwa wanafanya kazi kwa kujitoa zaidi malipo kidogo, lakini sasa malipo makubwa lakini kazi hazina ubora.
SOCIAL MEDIA ZETU:
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW
INSTAGRAM: @Globalpublishers
TWITTER: @GlobalHabari
FACEBOOK: @GlobalPublishers
SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers
GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz