Asalam Alaikum wapenzi wasomaji wa safu hii, bila shaka mnaendelea vema, walioharibikiwa mali kwa sababu ya mvua zinazoendelea kunyesha nawapa pole Mwenyezi Mungu awape subira na pia awape vingine Ishallah.
Leo kwenye safu hii nimekuja kuongea na akina mama wazee wenzangu ambao wanahisi uzee ndiyo mwisho wa maisha, kujipenda, kuvaa vizuri, kupaka rangi ya mdomo, kuonekana ng’aring’ari na kila kitu .
Kinachonituma kuongelea hili suala ni baba mmoja ambaye alinipigia simu na kuniambia kuwa ana miaka 43 kwenye ndoa yake na mkewe ambaye alianza naye uhusiano tangu wakiwa vijana, akasema kuwa kila siku zinavyozidi kwenda mkewe amekuwa tofauti, hajijali tena kama alivyokuwa kijana, ukimuuliza kwa nini anakwambia uzee anaona aibu.
“Mke wangu anatumiwa manukato, nguo na vyote vinavyohusika na urembo na watoto walioko Ulaya lakini havitumii, nikimuuliza mbona mama wewe ni mtu mzima na bado una mvuto mpaka leo hii, anaishia kunijibu tu amekuwa mzee, kiukweli mama hili jambo mimi linanishangaza sana simuelewi,” alisema msomaji huyo.
Alisema kuwa akimuuliza ni kwa nini anashindwa kupendeza kama zamani anamwambia kuwa anaona aibu kwa sababu wapangaji wanamcheka na kumwambia kuwa yeye ni mtu mzima kujipamba na kuvaa mavazi ya kumuonesha mrembo ni kujilinganisha na watoto.
Hili mimi kama mtu mzima nalipinga kwa asilimia kubwa kabisa, wapenzi wanawake wenzangu uzee mwisho Chalinze mjini kila mtu baby, kwa nini ujione umezeeka kwa kutopaka rangi ya mdomo, kutopendeza na kunukia?
Mwanamke kupendeza bwana, kumbuka ni maadili ambayo unaelezwa hata unapokwenda kwa mume, kupendeza ni kionjo kimojawapo ambacho kinamshawishi mumeo kuwa karibu na wewe.
Kwanza kumbuka ukipendeza mume anakaribisha wivu ambao si rahisi kukuacha na kwenda kujiachia nje kiurahisi hata kama atakwenda atarudi kwani kuna kitu kitamvuta tu kwako.
Sasa wewe ambaye unaamua kujiachia kisa umezeeka na unaona aibu huku mumeo anapenda kumbuka kuwa ndiyo unampa nafasi ya kwenda kutafuta anayependeza nje, wanawake ni tofauti na wanaume, wanaume huwa hawazeeki na hata wakizeeka huwa hawajiachii kama wewe mwanamke sasa iweje unapewa fursa na mumeo unaikataa?
Mwanamke ukipendwa pendeka hata kama umezeeka, hivi hamjifunzi kwa wenzetu Wazungu? Mwanamke anakuwa smati mpaka anazeeka na anaonesha mahaba kwa mumewe mpaka mwisho, yale yote aliyokuwa akiyafanya ujanani anayaenzi kama kawa.
Sisi Wabongo ukishafikisha miaka 45 tu ndiyo unaanza kunuka mdomo kwa ugoro, unashindwa kuvaa ukapendeza utasikia
siku hizi sivai nawaachia watoto, utamkuta mwanamke anavaa nguo wiki nzima anaivua kulala tu na kesho anaivaa tena. Akiwa anatoka anapenda nguo moja tu mpaka watu wanamsema kwa kuirudia nguo hiyo kila siku, niwakumbushe wanawake wenzangu wanaume hawapendezwi na mambo hayo ndiyo maana utakuta watu wazima wengi wanaume wanachukua vibinti kwa sababu wao huwa hawakubaliani na hali za wake zao.
Nakusihi endelea kuwa smati mpaka unaingia kaburini utamfanya mumeo kukuona mpya kila siku pamoja na uzee ulionao.