×

17 wapinduka na trekta, wajeruhiwa!

Stori: Stephano Mango, Ruvuma Ijumaa:

Mtembea kwa miguu, mkazi wa Kijiji cha Hanga wilayani Namtumbo mkoani hapa, Bitnes Ngonyani amegongwa na trekta ambalo lilikuwa limefungwa tela lililokuwa limebeba watu 17 ambao wamenusurika kifo baada ya tela la trekta hilo kupinduka.

Akizungumza na gazeti hili, ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, ACP Zubery Mwombeji alisema kuwa ajali hiyo ilitokea hivi karibuni, majira ya saa 10:00 jioni katika barabara inayounganisha Vijiji vya Hanga na Kitanda.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na Yakini Ndogoro (29), Basiri Ngonyani (25), Costantine Ngonyani (25), Goodluck Komba (32), Ismail Ndogoro (50), Asili Mwangama (20), Erick Komba (20) na Sanifa Nyoni (18) wote wakazi wa Kijiji cha Kitanda ambao hali zao zilikuwa mbaya hivyo kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma.

Alisema manusura hao walilazwa kwa matibabu zaidi siku tisa wakitibiwa katika Zahanati ya Kijiji cha Kitanda na kuruhusiwa baada ya hali zao kutengemaa.

Alisema inadaiwa siku ya tukio, trekta lenye namba za usajili T535 CWL, aina ya SONALIKA lililokuwa likiendeshwa na dereva ambaye jina lake halijafahamika mara moja huku likiwa na tela lake ambalo lilikuwa na abiria 17 lilimgonga Bitnes na kumsababishia majeraha katika mwili wake.

ACP Mwombeji alisema kuwa baada ya kumgonga mtembea kwa miguu huyo lilipinduka na kusababisha majeraha kwa watu wote waliokuwa wamepanda trekta hilo ambapo kati ya watu hao 17, watu 9 walitibiwa katika Zahanati ya Kijiji cha Kitanda na kuruhusiwa.

Kamanda Mwombeji alisema kuwa, kwa sasa jeshi la polisi mkoani hapa linamsaka dereva wa trekta hilo aliyekimbia.

Leave a Comment