×

Ingekuwa siyo muziki… wangerushiana Ngumi

Andrew Carlos
…piga kimya wewe ndiyo hufahi kabisa huna maana,
Wabana pua kila siku mnarogana,
bibi yako alikwambia muziki kama binti,
Mbona unawachezea unawatema kama big g,
Mara Wema, mara Jokate, mara Penny…

Ni sehemu ya mistari katika Ngoma ya Muziki Gani iliyoimbwa na Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ akimshirikisha Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Katika ngoma hiyo iliyotokea kupendwa na mashabiki wengi kutokana na staili ya majibizano, Nay anasikika akisifia zaidi Muziki wa Hip Hop na kuuponda Bongo Fleva kuwa wengi wanaoimba wanabana pua na wanaimba ili wapate wanawake tu.
Majibizano yaliyofanyika katika ngoma hii kwa mtu ambaye huwafahamu mastaa hawa unaweza dhania ni kweli wana bifu kutokana na yanayoongelewa kuwa na ukweli ndani yake ambao mashabiki wao wamekuwa wakiwaona ama kuwasikia.

Mapenzi au Pesa (Diamond & Nay)
Ukiachana na ngoma hiyo, Nay alitoka na ngoma nyingine iitwayo Mapenzi au Pesa akimshirikisha yuleyule Diamond ambapo katika ngoma hiyo, Nay anasikika akisifia mapenzi pesa huku Diamond akisisitizia mapenzi kupetipeti.
Katika ngoma hiyo, kila mmoja anaamua kumchana mwenzake ukweli ambao mashabiki wao wanaujua ama kuusikia.
Kuna sehemu Nay anasema;

…Si unakumbuka kipindi kile, unatoka na Nenda Kamwambie,
Walisema una bonge la domo, eti leo handsome si uchokozi…
Katika kumjibu Diam-ond anasikika akimsema Nay alivyo-porwa mwanamke (Siwema) na kwamba mafundi wamemteka na kumuachia mtoto na katika kudhihirisha hilo mwisho wa ngoma hiyo anasikika mtoto akilia huku Diamond akimlazimisha Nay ampe nyonyo.

Nakuchana (Ben Pol & Jux)
Utamu wa kuchanana mwingine umeibuka kati ya mastaa wa R&B, Juma Khalid ‘Jux’ pamoja na Bernad Paul ‘Ben Pol’ kupitia Ngoma ya Nakuchana.

Ngoma hiyo imewaacha mashabiki midomo wazi kutokana na wawili hao kufanya kolabo yao ya kwanza tangu walipoanza muziki na pili mashairi yaliyomo yana asilimia kubwa ya kuambiana ukweli ambao ingekuwa siyo muziki wangeweza kurushiana ngumi.

Akizungumzia kisa cha ngoma hiyo, Ben Pol anasema kuwa lengo lake kubwa lilikuwa kufanya kolabo ya ngoma nyingine kabisa na Jux lakini kitendo cha kufika studio (Kwa Manecky) hawakuwa na idea ya ngoma gani waandike kisha warekodi.

Wakazubaa zaidi ya saa tatu ndipo wakaanza kutaniana udhaifu wa kila mmoja katika mambo mbalimbali na hapo ndipo wazo la kutengeneza ngoma ya Nakuchana likaja.
Ukisikiliza ngoma hiyo, Jux anaonekana akimsifu Ben Pol kwa kuimba lakini kwa upande wa mavazi akiwa hajui kuvaa. Ben anaamua kumjibu kuwa Jux anapenda sifa, yeye anaimba.
Katika mashairi, kuna sehemu Jux anamchokoza Ben Pol kwa kumwambia;
…Natafuta msanii wa kumsaidia,

Niambie video yako ya mwisho nani kakulipia…
Ben anamjibu;
…Nafanya shoo kila mwaka,
Wapi wewe unapata pesa,
Stori zako nimeshazipata,
Unalelewa na Vanessa….
Katika ngoma hiyo, Ben amewataja wasichana ambao kwa namna moja ama nyingine ni kweli Jux alishawahi kuwa nao na mwingine bado yupo katika uhusiano.

Kwa staili hiyo ya kupeana ukweli huo unaouma, yawezekana tungesikia wametwangana manguni lakini kwa kuwa ni suala la makubaliano ili watengeneze fedha, ndiyo maana tunaona kama sehemu ya burudani tu! Baada ya hao, nani watafuata katika kuchanana? Tusubiri!

Leave a Comment