Hivi umeshawahi kujiuliza kwa nini unataka kuoa au kuolewa? Ni kwa sababu rafiki zako wengi wameoa au kuolewa? Ni kwa sababu wadogo zako wote tayari wana ndoa zao isipokuwa wewe? Ni kwa sababu unataka urahisi wa kutimiza haja zako za kimwili?
Umewahi kujiuliza kwamba unaingia kwenye ndoa kwa sababu kweli unahitaji kuanzisha familia na kuwa na mwenzi wa maisha yako mtakayevumiliana na kupendana kwenye shida na raha, uzima na maradhi, umaskini na utajiri?
Kama hujawahi kujiuliza, hebu jiulize hivi sasa, lengo hasa linalokufanya utake kuingia kwenye ndoa (kama bado haupo kwenye ndoa) ni nini? Au kama tayari upo kwenye ndoa lakini hakuna amani kati yako na mwenzi wako, kila siku ni migogoro isiyokuwa na mwisho, jiulize nini hasa kilikufanya uingine kwenye ndoa?
Utashangaa kugundua kwamba wengi wanaingia kwenye ndoa kama fasheni tu, kwamba kwa sababu ni lazima mwanaume na mwanamke waoane na kuanzisha familia, basi na wao wanafuata mkumbo tu. Matokeo yake, ndoa za namna hii zinakosa uhai na ndiyo chanzo cha nyingi kuvunjika muda mfupi baada ya kufungwa au miaka kadhaa baadaye.
Jambo la msingi ambalo unapaswa kulizingatia kabla ya kuingia kwenye ndoa (kama bado hujaingia) ni upendo wa dhati. Hata vitabu vya dini vinaeleza kwamba upendo una nguvu kuliko mauti.
Unapompenda mtu kwa dhati, utakuwa tayari kuachana na mambo mengine yote na kushikamana naye kujenga ndoa itakayokuwa bora na itakayodumu. Lakini kuwa na upendo pekee haitoshi kuwa sababu ya kuingia kwenye ndoa, jambo lingine muhimu ni dhamira ya dhati.
Je, moyo wako unahitaji kweli kuingia ndani ya ndoa na upo radhi kukabiliana na yote utakayokumbana nayo ndani yake? Kama jibu ni ndiyo, basi upo tayari kuingia kwenye ndoa. Jambo ambalo watu wengi huwa hawalielewi, ndoa siyo kitu cha kukifanyia mzaha au majaribio, ‘kwamba ngoja niingie nione itakuwaje!’
Ni lazima ujiridhishe sana kuhusu huyo unayeenda kuanzisha naye maisha ya ndoa. Utashangaa kugundua kwamba watu wanaingia kwenye ndoa lakini bado wanaendeleza zile tabia za ujana kama walizokuwa nazo kabla hawajaingia kwenye ndoa.
Wewe ni mke wa mtu tayari, una sababu gani ya kuvaa mavazi yanayoudhalilisha utu wako? Una haja gani ya kukesha baa na marafiki huku ukimuacha mwenzi wako akipigwa na baridi? Una sababu gani kutwa nzima upo kwenye mitandao ya kijamii, unachati na kuwasiliana na watu wa jinsia tofauti au kuposti picha zinazoshusha hadhi ya mwenzi wako?
Umeshaingia kwenye ndoa, kwa nini unaendelea kuambatana na marafiki hata wasiojua maana au thamani ya ndoa? Kwa nini huachi tabia za ‘ujana’? Unataka uende disko na marafiki mpaka usiku wa manane, unataka uendelee kupigiana simu na marafiki wa jinsia tofauti na yako kwa sababu tu mlisoma pamoja au mnafanya kazi pamoja?
Sisemi kwamba unapoingia kwenye ndoa basi ndiyo uwe mtumwa, hapana! Kuna baadhi ya vitu unapaswa kuvipunguza sana au kama havina maana ni bora ukaviepuka ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima.
Upo usemi wa masihara maarufu mitaani kwamba ndoa ndiyo mtihani pekee ambao unapewa cheti kabla ya kuingia kwenye chumba cha mtihani! Ukiamua kuingia kwenye ndoa, achana na mambo ya ujana, utaifurahia ndoa yako.