Haidary Gulamali.
DAR ES SALAAM: Wamefunguka! Kufuatia kamatakamata ya wafanyabiashara wanaodaiwa kuficha sukari na hivyo kuifanya kukosekana mitaani ambapo baadhi ya wauzaji wakubwa wamekamatwa wakidaiwa kufanya hujuma hiyo, wananchi wamefunguka ya moyoni, AMANI limeongea nao.
Wakiongea na gazeti hili mwanzoni mwa wiki hii, baadhi ya wananchi walitoa dukuduku lao wakisema kuwa wanashangazwa na jamii ya wafanyabiashara waliodaiwa kuficha sukari kuwa ni wenye asili ya Bara la Asia.
Rais John Magufuli
WASIKIE WABONGO
“Jamani! Kwani hawa Waasia si wenzetu? Mbona wao wanaonekana kuhusika zaidi? Mimi sisemi kwamba nawatenga, ila nashangaa kwa nini wao ndiyo sehemu kubwa,” alisema mama Ibra, mkazi wa Kimara Kibo, Dar.
Mkazi mwingine wa Ubungo-Makuburi, Dar aliyejitambulisha kwa jina la Salome Msigani, yeye alisema:
“Tumekuwa na undugu na hawa wenzetu kwa miaka nenda rudi. Wanakuja nchini tunawapokea kwa sababu tunawapenda, lakini baadhi yao naona wamekuwa hawatupendi.
“Angalia wanaodaiwa kuficha sukari, sehemu kubwa ni wao. Ni kwa nini lakini? Kama wanaamini sisi ni ndugu zao, waishi sawasawa na maagizo na serikali yetu ili tuzidi kupendana na kuondoa uwezekano wa kuhisiana vibaya zaidi. Nawaomba wasituone wanyonge sana, ila wajue wao ni wenzetu siku zote,” alisema Salome.
Mfanyabiashara, Haruni Zacharia.
KUTOKA ARUSHA
Mkazi mwingine wa Mbauda jijini Arusha, Jumanne Masimenti ambaye aliongea na gazeti hili kwa njia ya simu, yeye alisema:
“Naumia sana kuona watu wanaodaiwa kuficha sukari karibu wote wana asili moja, lakini sitaki kabisa kukubaliana na akili zangu kwamba wanafanya hivyo kwa sababu ya jinsi walivyo, sitaki. Najua wao na sisi ni sawa. Ila naamini waliokumbwa na madai hayo ni wao tu na si msimamo wa wenzao wote tunaoishi nao vizuri hapa nchini.
“Ninachotaka kusema zaidi ni kutaka kauli za Rais John Magufuli ziheshimiwe na kila mtu, awe Mbongo mwenye asili ya Asia, awe Mbongo mwenye asili ya Mbeya, wote wajue Magufuli kwa sasa ndiye rais wa nchi hii.
“Katika kauli zake, Magufuli amekuwa akisema yeye atawatumikia Watanzania wote bila kujali Chadema, CCM, Cuf wala chama kingine chochote cha siasa. Sasa na wao waige mfano wa rais wa nchi, wafanye biashara kwa kuwasadia Watanzania wote bila kujali rangi wala kabila.”
WAPONGEZA KUUNDWA KWA ‘EWURA’ YA SUKARI
“Mimi naipongeza serikali kuamua kuunda Ewura ya sukari kama ilivyounda Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) na kudhibiti bei ya mafuta nchini. Hii itasaidia kudhibiti hali hii siku za mbele kwani kuachia matokeo yake ni kuwafanya wachache watajirike na kutikisa nchi katika hali kama hii.”
TUMEFIKAJE HAPA?
Hivi karibuni, Rais John Magufuli aliwataka wafanyabiashara wakubwa wa sukari nchini kuuza bidhaa hiyo ili kuondoa uhaba uliojitokeza mitaani. Lakini akawaonya wale wenye sukari lakini wameifungia kwenye maghala huku akivitaka vyombo husika kuwasaka wafanyabiashara wenye tabia hiyo.
Siku moja baada ya kauli hiyo ya mheshimiwa rais, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) jijini Dar es Salaam ilikamata shehena ya sukari kwenye ghala lililopo Tabata ikidaiwa ni mali ya mfanyabiashara, Haruni Zacharia.
Sakata hilo likazidi kupata mapana yake karibu sehemu mbalimbali za nchi ambapo wafanyabiashara wengi waliendelea kukutwa wakiwa wameficha sukari.
Kwa hiyo mpaka sasa, wafanyabiashara ambao wameshafikiwa na vyombo vya dola kwa kukaguliwa kisha kuhojiwa ni kwa tuhuma za kuficha bidhaa hiyo muhimu, ni Zacharia anayemiliki Kampuni ya Al Naeem, (tani 4,579.2) katika maghala ya Tabata, Dar.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wachunguzi wa taasisi hiyo na wa Jeshi la Polisi Tanzania walifanya ukachero wao katika maghala ya kampuni hiyo yaliyopo Mbagala na Tabata, Mei 5, mwaka huu.
Mkoani Morogoro, mkuu wa mkoa huo, Kebwe Steven Kebwe aliagiza kufuatiliwa kwa mfanyabiashara Sadick Yassin ambaye alifunga duka lake wakati wa ukaguzi.
Baadhi ya wauzaji wa maduka ya jumla waliokaguliwa na timu ya mkuu wa mkoa ni Thabit Islam na Hassan Binzoo ambao walisema hali ya upatikanaji wa sukari katika kipindi hiki ni ngumu kutokana na kuadimika ghafla.
Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, polisi ilifanya upekuzi katika baadhi ya maghala ya kuhifadhia sukari na kuwabaini wafanyabiashara wanne.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana aliagiza tani 154 kuuzwa kwa wananchi kwa bei elekezi huku akiwataka wafanyabiashara ambao bado wameficha sukari kuitoa mara moja kabla rungu halijawashukia.
Takukuru kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani hapo walikamata na kuzifungia tani 154 za sukari katika ghala la mfanyabiashara Haidary Gulamali aliyesema ana vibali vyote.
Mkoani Lindi, TRA mkoani humo imegawa sukari ya magendo mifuko 5,319 yenye thamani ya Sh. 373,521 kwa taasisi mbalimbali za mkoani humo baada ya kuthibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuwa ni salama.
Sukari hiyo ilikamatwa Februari, mwaka huu, katika Bandari ya Lindi ikiingizwa nchini kinyume cha sheria kutoka Brazil kupitia Bandari ya Zanzibar na imegawiwa kwa shule za sekondari, magereza na ofisi ya mkuu wa mkoa.
KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP
*********
JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU:
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA
INSTAGRAM: @Globalpublishers
TWITTER: @GlobalHabari
FACEBOOK: @GlobalPublishers
SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers
GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

