MARA baada ya Yanga kufuzu Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, bosi wa benchi la ufundi la klabu hiyo, Hans van Der Pluijm, amefunguka kuwa, anataka kuhakikisha timu hiyo inafika mbali na moja ya mikakati yake ni kuongeza wachezaji kadhaa katika kikosi chake kabla ya hatua hiyo.
Wakati akisema hayo, Pluijm amesisitiza kuwa kwa levo ambayo Yanga imefikia, hana hofu dhidi ya timu yoyote katika hatua hiyo kwa kuwa Al Ahly ya Misri ni moja ya timu bora Afrika lakini wao Yanga waliwapa wakati mgumu walipokutana na ndiyo maana anaamini kikosi chake kipo tayari kwa mpinzani yeyote.
Yanga imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa Sagrada Esperanca kwa jumla ya mabao 2-1, ambapo Pluijm amesisitiza kuwa usajili ni muhimu ili kuongeza nguvu kikosini hapo kuelekea katika hatua hiyo ambapo kuna timu kadhaa vigogo zikiwemo TP Mazembe ya DR Congo na Étoile du Sahel ya Tunisia.
“Tulicheza dhidi ya Al Ahly, walikuwa wazuri na kila mtu aliona ilivyokuwa tulipocheza nao, ndiyo maana naona sina hofu yoyote,” alisema Pluijm baada ya kuulizwa juu ya utayari wake katika hatua inayofuata.
“Yanga tupo vizuri, tumeshindwa kupata ushindi katika mechi ya huku (Angola) kwa kuwa wapinzani wetu walikuwa wakicheza mipira mirefu na wakawa wengi kila wanapokuwa mbele ya mabeki wetu.
“Tunapokutana na timu ambayo ipo tayari kucheza mpira nasi huwa tunacheza soka zuri, hawa wapinzani wetu (Sagrada) walikuwa na mbinu zao za ajabu,” alisema Pluijm.
Kuhusu usajili mpya hakuwa tayari kuzungumzia kiundani zaidi ya kusema kuwa amekuwa akipata tabu kusajili wachezaji kutoka Tanzania katika nafasi na ubora ambao anauhitaji.
Pluijm aliongeza kuwa kilichotokea Angola katika mchezo wao wa pili dhidi ya Sagrada ni funzo kubwa kwao na kwa Watanzania, hasa kuhusu timu zao.
Aidha, Pluijm alimzungumzia mwamuzi wa mchezo huo wa Angola, Hamada el Moussa wa Madagascar, kwa kusema:
“Baada ya mchezo nilimfuata na kumwambiwa alichokuwa akikichezesha uwanjani kilikuwa cha ajabu, alitoa maamuzi mengi ambayo hayakuwa sahihi.”
Wakutana na refa kwenye ndege
Katika mchezo huo, mwamuzi alionekana kuwa upande wa wenyeji, ikiwemo kutoa penalti yenye utata ambayo walikosa pamoja na kumpa kadi nyekundu nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Wakati wakiondoka jijini Luanda, wachezaji wa Yanga walipanda ndege moja na mwamuzi huyo na wenzake, mara baada ya kumuona wachezaji wa Yanga wakataka kumfuata lakini viongozi wao waliwakataza, wachezaji hao wakatii amri hiyo.
Cannavaro: Sijawahi kucheza mechi ngumu kama hii
“Huu mchezo ulikuwa mgumu sana, sikutegemea kama ungekuwa hivi ulivyokuwa lakini mwamuzi hakuwa ‘fea’, aliwabeba Sagrada na hata kadi yangu haikuwa sahihi.
“Tunashukuru tumesonga mbele lakini wametupa funzo kuwa tunatakiwa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani,” alisema beki huyo.
Yanga watoa tamko, walaani
Kutoka jijini Dar es Salaam, Klabu ya Yanga ilitoa tamko juu ya vurugu zilizotokea katika dakika za mwisho za mchezo huo na kusababisha askari kuingia uwanjani na kusababisha mvurugano wa hapa na pale.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro alisema wanalaani vurugu hizo na matukio mengine ya kuwatisha wachezaji.
“Tumepanga kuwashitaki waamuzi waliochezesha kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) pia tutawashitaki Sagrada kutokana na figisu walizotufanyia kwa kuwa matukio kama hayo siyo ya kwanza kutokea, yalitokea pia kule tulipocheza na Al Ahly.
“Tunaomba serikali ya Rais (John) Magufuli itusaidie kuhusu masuala ya usafiri ikiwezekana tuwe tunapewa ndege ya serikali na sisi kulipia gharama za mafuta kama itawezekana,” alisema Muro.
Waomba fainali isogezwe mbele
“Timu itawasili leo mchana, ikifika moja kwa moka kambini, kisha Jumamosi (kesho) tutasafiri kwenda Ruvuma kwa ajili ya mechi dhidi ya Majimaji (Jumapili, baada ya mechi Jumatatu timu itarudi Dar kujiandaa na mechi ya Jumatano ya fainali dhidi ya Azam FC (Kombe la FA).
Ratiba imetubana sana, tunaomba kama kuna uwezekano mchezo wetu huo usogezwe mbele kwa kuwa wachezaji hawatapata muda wa kupumzika.
Swadaktah