×

‘Samahani mpenzi’ zikizidi, huyo hakufai!-2

Couple ignoring each other --- Image by © Lou Cypher/Corbis
Couple ignoring each other — Image by © Lou Cypher/Corbis

Karibu msomaji wa makala haya pia niwatakie mfungo mwema ndugu zetu Waislamu wote duniani kwani mfungo wa Ramadhani ni mmoja ya nguzo muhimu sana katika dini ya Kiislamu.

Karibuni katika muendelezo wa mada iliyopo hapo juu, ambayo tulianza nayo wiki iliyopita. Kuna hili suala la kukosewa na mpenzi wako kisha akakuomba samahani. Hili katika mapenzi linakubalika kabisa kwani kila siku tunakoseana na samahani ndilo neno linaloweza kurudisha amani katika penzi.

Kuna watu ni wagumu sana kuomba msamaha. Yaani wanajua wamekosa lakini wanaona kuomba msamaha ni kujishusha. Hii ni mbaya sana na inaweza kusababisha kupunguza mapenzi kati ya wawili waliotokea kupendana.

Pia kuna ambao ni wagumu kusamehe. Yaani mpenzi wake kafanya kosa kwa bahati mbaya na anagundua amekosea lakini akiomba msamaha, hasamehewi. Hili nalo ni tatizo!

Ila sasa kuna watu ambao kila siku ni samahani tu. Wapo ambao kila siku wanakosewa na wapenzi wao na kuishia kuombwa msamaha. Hili kimsingi ni jambo linaloweza kuleta picha ya tofauti.

Tunachojua ni kwamba, unafanya kosa leo, unaomba msamaha na kutorudia tena kosa. Lakini kama leo unamsaliti mwenzako, anakusamahe, kesho tena unasaliti, kwa kuwa anakupenda anakusamehe, keshokutwa tena unarudia kosa lilelile, katika mazingira hayo ni kweli unastahili kuendelea kusamehe?

Sidhani kama inakuja! Kurudia makosa yaleyale kwa kutarajia kuwa utaomba msamaha na kusamehewa ni kuonesha kwamba unamdharau mwenzio na kimsingi kama utakuwa ni mtu wa ‘samahani mpenzi’ kila siku na hubadiliki, hiyo ‘samahani’ yako haitakuwa na faida.

Ninachoweza kusema ni kwamba, kama huyo uliyenaye unampenda kwa dhati, anaweza kukukosea mara nyingi kwa makosa mbalimbali na ukaendelea kumsamehe bila kuchoka kwa kuwa unampenda na hauko tayari kumkosa kwa makosa yanayosameheka.

Lakini kama mpenzi wako atakukosea makosa mawili-matatu kisha ukafanya maamuzi ya kumuacha, utakuwa unadhihirisha kwamba, hukuwa na mapenzi ya dhati kwake na ndiyo maana kakukosea mara moja au mbili, ukaona ndiyo mwanya wa kumpiga kibuti.

Tujenge utamaduni kwa kusameheana kwani hakuna aliyekamilika kwa asilimia 100 na ndiyo maana kila siku tunakoseana.

Lakini kama kila siku wewe umekuwa wa kumkosea tu mwenzio na kuomba msamaha, unasamehewa hilo ni tatizo na hata neno msamaha lenyewe linakuwa halina maana kwako na kwa mpenzi wako.

Wapenzi wengi wamekuwa wanalalamika kwa kuachwa na wapenzi wao au kutokudumu na wapenzi wao wakati sio wasaliti, wao wanaamini kosa ni usaliti tu si kweli hata makosa madogo madogo yanakwaza na yanaweza yakauvuruga vibaya uhusiano wako.

Jifunze kuwa muelewa, unapokosea na kusamehewa basi jirekebishe laasivyo utawaona wanaume au wanawake wote ni walewale na wakorofi kumbe ukweli ni kwamba wewe ndiyo siyo mstaarabu, hutumii hekima katika kuchanganua jambo.

Kwa ushauri na maoni tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Ista:mimi_na_uhusiano au jiunge kwenye group letu la WhtsApp kwa namba iliyopo juu.

Leave a Comment