JUZI mtu wangu mmoja wa karibu alinipigia simu na kuniuliza kama katika wiki hizi mbili na nusu zijazo bado anaweza kununua kuponi na kushinda, maana anaamini kama amechelewa, nikamjibu hajachelewa na kwa kuwa nadhani watu wengi pia wana swali kama hilo, nikaona ni busara kuwajibu kupitia ukurasa huu.
Nyumba hii kubwa, yenye thamani ya shilingi milioni 60, iliyopo maeneo ya Salasala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, haitembei. Haitembei kiasi cha wewe kudhani labda hautaikuta. Hapana, mjengo upo pale unakusubiri wewe.
Kama kuna mtu atakuwa amechelewa, basi huyo ni yule atakayeulizia nyumba baada ya siku za shindano kumalizika, yaani Juni 30, mwaka huu, vinginevyo, bado upo ndani ya wakati.
Sifahamu kuhusu wengine, lakini mimi huwa nina imani moja, kwamba ninapenda kuwa nyuma, yaani kama tunaingia ndani ya gari, napenda niingie mwisho ili nikakae mwishoni, maana watu wengi hupenda kukaa mbele.
Kama ningekuwa nashiriki shindano hili, ningenunua kuponi hizi za mwishomwisho kwa sababu ninaamini hizi ndizo zitakaa juu. Ninaona kama vile hizi kuponi zote zitaingia kwenye pipa moja kuuuubwa, sasa zile za zamani zimetangulia chini.
Ninaamini kwa kuwa hizi zitakuwa juu, basi uwezekano wa kuponi yangu kunyakuliwa na muokota kuponi ili nitangazwe mshindi ni mkubwa sana kuliko wale wa mwanzo.
Zoezi la kukata na kujaza kuponi za shinda nyumba
Nikushauri uwe na imani kama yangu na kwa maana hiyo, huu ndiyo wakati muafaka wa kuhakikisha haukosi nakala ya magazeti ya Global Publishers ambayo yatakuwezesha kushinda zawadi kubwa kabisa kuwahi kutolewa katika bahati nasibu zilizowahi kuchezwa Tanzania.
Hakikisha haukosi Amani, Championi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Risasi na Uwazi. Magazeti haya yote kasoro Ijumaa, yanauzwa kwa shilingi mia tano tu na lile la Ijumaa linauzwa kwa shilingi elfu moja, lakini likiwa limeboreshwa sana.
