×

RC Makonda Ayafanyie Kazi Haya

RC Makonda (2)

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda.

Na Leonard Msigwa

MWAKA 1918 wakati Vita ya Kwanza ya Dunia ikiwa imepamba moto, kiongozi wa Urusi, Vladimir Leninm alitembelea uwanja wa mapambano kuwapa morali wanajeshi wake. Kamanda mmoja akamwambia Lenin, “mkuu ni bora turudishe vikosi nyuma, askari wetu wanazidi kuangamia.”   Lenin alimjibu, “askari wa kweli ni yule anayeipigania nchi yake hadi mwisho.”   Hatimaye,  Jeshi la Urusi lilishinda vita.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda toka akabidhiwe jukumu la kuongoza jiji hilo maarufu amekuwa akitoa maagizo mengi yenye lengo la kuliweka jiji katika mwonekano wa kiustaarabu. Alianza kwa kupiga marufuku watu kutupa takataka, alizuia ombaomba na sasa kaja na agizo la kupiga marufuku ushoga na matumizi ya shisha.

Binadamu yeyote mstaarabu anaungana na Makonda, inawezekana wakawepo watu ambao hawakubaliani na agizo lake kama yule kamanda wa Urusi aliyemwomba Lenin warudishe jeshi nyumbani. Nguvu ya ziada inahitajika kuhakikisha maagizo hayo yanafanikiwa.

Makonda anapaswa kufanyia kazi mambo mengi kufikia malengo, baadhi ya masuala muhimu anayotakiwa kuyafanyia kazi ni haya yafuatayo;

Aimarishe sungusungu

Anapaswa aimarishe sungusungu kuhakikisha utekelezaji wa maagizo yake, anatakiwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha sungusungu wanakuwa imara maeneo yote yanayozunguka jiji lake. Hawa wanawajua mashoga, wanajua maeneo yanayovutwa shisha na inapouzwa, wanajua mitaa ya ombaomba pia wanajua vyema maeneo akina ‘dada poa’ wanapojiuza.

RC Makonda (1)

Paul Makonda akiwa na mama ombaomba pamoja na watoto wake. Mama huyu aliamua kurudi nyumbani kwao Ngara na kuacha kazi hiyo.

Morali ya posho na zawadi

Mkuu huyo wa mkoa anapaswa kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ili kufanikisha malengo yake. Morali ya posho na zawadi vitasaidia kuwapata wote wanaojihusisha na biashara hizo haramu. Mfano kama akiendelea kutoa nauli na mtaji kwa ombaomba ni dhahiri wengi watarudi makwao. Pia posho au zawadi hizo zitumike kuwalipa wale wote wanaotoa taarifa za siri kuhusiana na wote wanaokiuka maagizo yake.

Vijana wasio na ajira

Vijana wasio na ajira jijini ni wengi sana, hawa wakipewa semina na motisha wanaweza kufanikisha malengo yake kwa urahisi zaidi kuliko kutegemea askari wa jiji na polisi pekee. Hawa wapewe maeneo ya kufanya utafiti kuhusu ushoga, uchangudoa na uuzaji wa shisha,  watakuja na majibu yenye tija. Pia wana uwezo wa kucheza na mtandao kuwabaini wale wanaojitangaza kuwa ni mashoga kuliko kuwasubiri TCRA na polisi pekee.

Uwazi wa faini

Uwepo uwazi wa faini (sheria izingatiwe) kwa wale wote wanaokamatwa kujihusisha na vitendo hivyo, isitoshe kuwaambia wataadhibiwa bali iwekwe wazi ni faini kiasi gani wataadhibiwa. Faini siku zote hupunguza uharifu na matendo yasiyofaa katika jamii.

Kianzishwe kitengo maalum

Kianzishwe kituo maalum cha kupambana na biashara haramu ndani ya jiji, kwani majiji makubwa duniani yana vitengo maalumu mbali na jeshi la polisi. Vitengo hivi hujihusisha na kuzuia matukio hasa yale yasiyohitaji nguvu kubwa ya kijeshi kuyazuia. Hili linawezekana kama viongozi wote wa jiji wataungana.

Mwisho, elimu ya uraia inahitajika zaidi kwa makundi yote wahanga wa ushoga, ombaomba na umalaya. Lazima iwepo mikakati maalum ya kuwasaidia kwani kuwazuia pekee bila kuwapa elimu haitosaidia. Hawa ni sehemu ya jamii hawapaswi kutengwa bali wanatakiwa kuelimishwa na kuwasaidia mitaji kwa kuwadhamini na kuwapa elimu ya ujasiriamali.

“Inawezekana Dar es Salaam bila ushoga, bila uvutaji shisha na bila biashara ya umalaya!”

Leave a Comment